1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwongozo wa Umoja wa Ulaya wapinga ubaguzi

P.Martin30 Januari 2007

Azma ya mwaka wa usawa wa jinsia barani Ulaya,ni kuimarisha hisia za wakaazi wa nchi za Umoja wa Ulaya kuhusu haki ya kutendewa sawa sawa na pia kuwa na maisha yasio na ubaguzi.

https://p.dw.com/p/CHlh

Mkutano wa kilele wa siku mbili kuhusu usawa wa jinsia,uliofunguliwa siku ya Jumanne katika mji mkuu wa Ujerumani,Berlin unahudhuriwa na wajumbe 450 kutoka makundi mbali mbali ya kijamii.Makundi hayo yanajishughuliha na mwongozo wa Umoja wa Ulaya unaopiga marufuku ubaguzi kwa sababu za kidini,kijinsia,umri,ulemavu,maoni ya binafsi kuhusu siasa duniani au kwa sababu ya uhusiano wa kimapenzi kati ya watu wa jinsia moja.Mwaka jana,mwongozo huo ulijumuishwa katika sheria ya Ujerumani na kuanza kutumiwa tangu tarehe 18 Agosti mwaka 2006.

Kinyume na khofu zilizotamkwa hadhrani,hadi hivi sasa sheria hiyo mpya inayozuia ubaguzi, haikusababisha mfuriko wa malalamiko na mashtaka. Kwa mfano,idara inayohusika na sheria ya ubaguzi ambayo ilifunguliwa na wizara inayoshughulika na masuala ya kifamilia,imesema kuwa tangu Agosti 18 imepokea kama masuala 900 tu.Takriban asilimia 60 ya masuala hayo yametoka sekta tofauti,kama vile kutoka vyombo vya habari,jumuiya mbali mbali, waajiri na mashirika ya bima.Ni asilimia 40 tu ya masuala yaliyoulizwa yalitoka kwa watu walioathirika kwa ubaguzi.

Sehemu kubwa ya masuala hayo yalikuwa juu ya ubaguzi uliohusika na ulemavu na umri.Nafasi ya tatu imechukuliwa na masuala yaliohusika na ubaguzi wa kijinsia.

Kwa upande mwingine waajiri na mashirika yao hulalamika kuwa Ujerumani,ambayo tayari ina sheria za kuwalinda mama na walemavu,kinyume na ilivyo katika nchi zingine za Ulaya,imekwenda mbali zaidi kuliko mahitaji ya mwongozo wa Umoja wa Ulaya.Kwa maoni ya Hildegard Reppelmund anaehusika na masuala ya haki za ajira katika Baraza la Viwanda na Biashara la Ujerumani,bado kuna haja ya kufanywa marekebisho ili kuhakikisha haki zaidi.Ni matumaini yake kuwa wajumbe 450 kutoka Ulaya nzima wanaohudhuria mkutano wa siku mbili mjini Berlin,watatoa maarifa yao pamoja na mikakati na fikra mpya kuhusika na mada ya ubaguzi na nafasi ya kutendewa sawasawa.

Lakini kwa maoni ya kundi la wabunge wa kike wa vyama vya Ujerumani vya CDU na CSU,kwa sababu mbali mbali,hatua rasmi ya kuwapa usawa wanawake nchini Ujerumani haikuleta cho chote mahala pa kazini,kwani bado kuna tofauti kati ya mishahara ya wanaume na wanawake;vile vile ni wanawake wachache walio na vyeo vya juu au walio katika uongozi wa tabaka ya kati;na hata kazini bado kuna masharti tofauti yanayowahusu wanawake.