1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Myanmar kuwarejesha nyumbani Warohingya

Admin.WagnerD16 Januari 2018

Bangladesh na Myanmar zimekubaliana kutekeleza mpango wa kuwarejesha nyumbani mamia kwa maelfu ya wakimbizi wa jamii ya Waislamu wa Rohingya waliokimbia machafuko nchini Myanmar.

https://p.dw.com/p/2qvZV
Bangladesch Rohingya-Flüchtlinge in Palong Khali
Picha: picture-alliance/dpa/B. Armangue

Wizara ya mambo ya kigeni ya Bangladesh imesema jopokazi la pamoja kutoka nchi hizo mbili limekamilisha makubaliano jana kuhusu kurudishwa nyumbani kwa watu wa jamii ya Rohingya. Imesema nchi hizo zimekubaliana  kuwa mchakato huo utakamilishwa ikiwezekana ndani ya miaka miwili baada ya kuanza kutekelezwa.

Myanmar na Bangladesh zilisaini makubaliano ya awali mnamo mwezi Novemba kuwarejesha Warohingya, na jopokazi hilo la wanachama 30 liliundwa mwezi uliopita ili kuusimamia mchakato huo. Wengi wana maswali kama Warohingya wataweza kurejeshwa Mnyamar chini ya mazingira ya sasa, na kama Myanmar itawakaribisha na kuwakubalia kuishi kwa uhuru.

Chini ya makubaliano ya Novemba, Warohingya watahitaji kutoa ushahidi wa makazi yao nchini Myanmar ili kurejea makwao – kitu ambacho wengi wanasema hawana.

Rohingya-Hochzeit im Flüchtlingscamp
Warohingya wanaishi katika mazingira magumuPicha: Reuters/M. Djurica

Taarifa kutoka wizara za mambo ya kigeni za Myanmar na Bangladesh zimesema Bangladesh itaweka kambi tano za muda kwenye upande wake wa mpaka. Kambi hizo zitatumiwa kuwapeleka Warohingya katika vituo viwili vya kupokelewa nchini Myanmar. Mchakato huo wa kuwarejesha makwao utaanza Jumanne wiki ijayo.

Myanmar imesema itajenga kambi ya muda inayoweza kuwahifadhi wakimbizi 30,000 watakaorejea nyumbani

Myanmar imesisitiza haja ya pande zote kuchukua hatua za kuzuia uwezekano wa kufanyika mashambulizi mengine ya Rohingya na ikasema imeipa Bangladesh orodha ya majina 1,000 ya watu wanaodaiwa kuwa wanamgambo

Zaidi ya Warohingya 650,000 wamekimbilia Bangladesh tangu mwezi Agosti, wakati jeshi la Myanmar lilipoanzisha msako mkali katika jimbo la Rakhine baada ya kundi moja la wanamgambo kuvishambulia vituo vya polisi.

Jeshi linakanusha kuhusika na safishasafisha ya kikabila likisema vikosi vyake vilifanya operesheni halali za kupambana na uasi.

Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Wakimbizi – UNHCR amesema Warohingya wanapaswa tu kurejea makwao kwa hiari wakati watakapohisi ni salama kufanya hivyo.

Msemaji wa serikali ya Myanmar aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa watakaorejea nyumbani wanaweza kuomba uraia "baada ya kuupitia mchakato wa uhakiki”.

Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Human Rights Watch barani Asia Phil Robertson anasema makubaliano hayo hayakuangazia hofu na wasiwasi wa wakimbizi wenyewe. Anasema hakukuwa na masuala ya ulinzi wa Warohingya dhidi ya vikosi vya usalama vya Myanmar ambavyo miezi michache iliyopita vilituhumiwa kwa ubakaji na mauaji

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga