1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Myanmar yabadili baraza la mawaziri

28 Agosti 2012

Myanmar imefanya mabadiliko katika baraza la mawaziri ikiwa ni hatua mojawapo kuelekea kwenye mageuzi ya kisiasa.

https://p.dw.com/p/15xoh
Picha: Reuters

Mabadiliko hayo yamewaweka washirika wake wa karibu kwenye vitengo muhimu na kuwaondoa baadhi ya mawaziri waliokuwa kwenye utawala wa zamani wa kijeshi.

Hatua hii iliyofikiwa na Rais Thein Sein wa nchi hiyo imekuwa ikisubiriwa kwa hamu kwa muda mrefu. Mawaziri tisa kwenye baraza la zamani wamebadilishiwa majukumu katika mageuzi hayo.

Jumuiya ya kimataifa inaitazama hatua hii kama alama ya kufanya kazi kwa sera mpya za rais Sein zinazolenga kuimarisha nguvu zake na kuibadili Myanmar kuwa taifa la kidemokrasia.

Generali wa zamani Sein amewapa mawaziri wanne muhimu katika safu yake ya mawaziri nafasi za kuwa mawaziri katika ofisi ya rais katika kile ambacho wasaidizi wake wanasema kuwa njia ya kuharakisha mageuzi ya kisiasa.

Mawaziri wa karibu yake kuwa chini ya Rais

Mawaziri hao ni pamoja na wa usafiri Aung Min ambaye amekuwa na mchango mkubwa katika mazungumzo ya amani utawala na makundi ya kikabila pamoja na waziri wa fedha Hla Tun na waziri wa viwanda Soe Thein ambaye ni mtu muhimu kwenye masuala ya uchumi.

Marekani na Umoja wa Ulaya zilisitisha vikwazo vya kiuchumi dhidi ya nchi hiyo baada ya kuonyesha nia ya kutaka kufanya madabadiliko kwenye siasa zake ambazo kwa kiasi kikubwa zilikuwa ni za ukandamizaji. Mawaziri tisa katika baraza la zamani wamebadilishiwa majukumu.

Rais Thein Sein wa Myanmar na waziri wa mambo ya kigeni wa Mrekani Hillary Clinton
Rais Thein Sein wa Myanmar na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary ClintonPicha: AP

Afisa wa serikali amesema kuwa mawaziri hao watafanya kazi ya kumshauri Rais Sein na yeye kazi yake itakuwa ni kufanya maamuzi ya mwisho tu na hivyo atapata muda zaidi wa kuyashughulikia masuala mengine muhimu akiongeza kuwa majina ya watakaorithi nafasi zilizoachwa wazi na viongozi hao yatatolewa baadae.

Mabadiliko Myanmar

Tangu achukue hatamu ya uongozi mwaka uliopita, Thein Sein ameshuhudia mabadiliko mengi katika siasa za nchi hiyo ikiwemo kuwaachia mamia ya wafungwa wa kisiasa na kuchaguliwa kwa kiongozi wa upinzani Aung Suu Kyi kuwa mbunge.

Raia nchini Myanmar
Raia nchini MyanmarPicha: dapd

Hata hivyo kumekuwa na dalili za wasiwasi baina ya wafuasi wa mtazamo wa mabadiliko ya kisaisa ndani ya serikali na wahafidhina wanaopinga mabadiliko ya haraka katika siasa za nchi hiyo.

Mabadiliko hayo yanafanyika ikiwa ni wiki moja tu baada ya Mynmar kutangaza kuwa imesitisha utaratabu wa kuvibana vyombo vya habari ambao hapo kabla ulikuwa ndio mtindo wa maisha chini ya utawala wa kijeshi uliodumu kwa takribani miaka 50 kabla ya kuondolewa mwaka jana.

Tukio lilifuatiwa na uteuzi wa mkuu wa vikosi vya jeshi la majini kushika nafasi mojawapo ya makamu wa rais hatua ambayo wachambuzi wanasema ni kuimarisha nguvu kwa viongozi wanaoshiriki katika mabadiliko ambayo nchi hiyo inapitia.

Kiongozi wa upinzani nchini Myanmar, Aung San Suu Kyi
Kiongozi wa upinzani nchini Myanmar, Aung San Suu KyiPicha: dapd

Kuna uvumi kuwa huenda Suu Kyi naye akapewa nafasi kwenye baraza hilo jipya, lakini yeye mwenyewe amesema hakuna uwezekano ho kwa kuwa akipewa nafasi hiyo itamlazimu kuachia nafasi yake ya ubunge kwa mujibu wa katiba ya taifa hilo.

Mwandishi: Stumai George/AFP

Mhariri: Yusuf Saumu