1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzee Msalaba Masongi awaajiri vijana Shinyanga

23 Machi 2016

Mzee Msalaba anamiliki Kiwanda cha kutengeneza vitu vya chuma kama vile injini za mashine za kusaga, baiskeli, mikokoteni na bidhaa nyingine. Mwandishi wetu wa Shinyanga Veronica Natalis aliitembelea karakana hiyo.

https://p.dw.com/p/1IIPU
Tansania Workshop in Shinyanga
Mzee Msalaba akionyesha jinsi mashine ya kuchomelea vyuma inavyofanya kaziPicha: Veronica Natalis

Kiwanda cha kutengeneza vitu vya chuma kama vile injini za mashine za kusaga, baiskeli, mikokoteni na bidhaa nyingine ni kiwanda kinachomilikiwa na mtu binafsi mwenye ujuzi wa ufundi alioupata kutoka kwa mafundi wengine na baadaye kujifunza chuoni kwa kipindi cha miaka mitatu. Mzee Msalaba Masongi.

Kiwanda hicho ambacho muonekano wake ni wa kawaida kwani kimejengwa kwa miti na mifuko ya plastiki, kilianzishwa mwaka 1999 na tangu kuanzishwa kwake kimeweza kutoa mafunzo hayo ya ufundi kwa vijana zaidi ya 100 ambao wameajiriwa na kujiajiri maeneo mbali mbali ya Tanzania.

Msalaba Masongi anasema alianza kujifunza kutengeneza vifaa vya vyuma mwaka 1971 kwa kuwatembelea mafundi wengine na ndipo hapo alipochukua utaalamu, na wakati huo bidhaa zilizokuwa zikitengenezwa sana ni majiko ya kupikia yanayotumia mkaa. Mwaka 1973 alifungua ofisi yake wakati huo akiwa na vitendea kazi vitatu tu.

Mafunzo ya Morogoro

Mwaka 1975 mwalimu Julius kambarage Nyerere akiwa rais wa Tanzania kwa kipindi hicho alianzisha mpango wa kuwakusanya mafundi wenye ujuzi kidogo wa kutengeneza vifaa vya vyuma na kuwapeleka katika chuo cha ufundi mkoani Morogoro kwenda kuwaongezea ujuzi ili baadaye wapelekwe wakayasaidie mashirika ya kuhudumia viwanda vidogo nchini Tanzania yajulikanayo kama SIDO. Msalaba alikuwa ni miongoni mwa watu waliobahatika kupata mafunzo hayo katika chuo cha ufundi MANGH'ULA mkoani Morogoro.

Tansania Workshop in Shinyanga
Karakana ya Mzee Msalaba, Shinyanga, TanzaniaPicha: Veronica Natalis

Baada ya mafunzo hayo aliajiriwa na shirika la nyumba la taifa, Tanzania Nation Housing Cooperation, na akafanya kazi kwa mwaka mmoja. Baadaye akaona ni vyema kufungua kiwanda chake cha kutengeneza vifaa vya vyuma, kwa sasa anatengeneza injini za mashine za kusaga, anatengeneza baiskeli, mikokoteni na bidhaa nyingine nyingi. Anajivunia kazi hii kwani inamuingizia kipato cha kuihudumia familia yake yenye watoto saba kando na hilo ameweza kufundisha vijana zaidi ya 100 ujuzi wa ufundi ambao nao wamejiajiri na kuajiriwa maeneo mbali mbali ya Tanzania.

Mashaka Msalaba ni miongoni mwa vijana waliopata mafunzo katika kiwanda hicho ambapo anasema ugumu anaokutana nao ni upatikanaji wa malighafi. Pamoja na yote hayo Msalaba anahitaji kupata vitendea kazi vya kisasa ili kuboresha kazi yake.

Mwandishi:Veronica Natalis

Mhariri:Josephat Charo