1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

mzozo Darfur watimiza miaka sita leo.

Nyanza, Halima26 Februari 2008

Mzozo wa Darfur umetimiza miaka sita tangu ulipozuka, ambapo mpaka sasa bado haijapatikanasuluhu, huku serikali ya Sudan ikiendelea kupinga kutawanywa kwa kikosi kamii cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/DDf0
Walinzi wa kulinda amani wa China, wakiwa katika ujenzi wa kituo cha U.N. huko Darfur, Sudan.Picha: AP

Maadhimisho hayo yanakuja wakati mjumbe maalum wa Marekani kwa Sudan, Richard Willliamson na wa China katika eneo la Darfur Liu Giujin, wakiitembelea Sudan kwa mazungumzo ya ngazi ya juu yaliyokuwa na lengo la kupatia ufumbuzi mzozo huo.

Rais wa Marekani George w Bush, alisema kuwa mauaji ya halaiki yanaendelea kutokea katika jimbo hilo la Darfur, wakati China imekuwa ikilaumiwa kutoa silaha nyingi ambazo hutumika kuangamiza askari waasi, wakati huohuo China ikidaiwa kufumbia macho juhudu za kidiplomasia katika, kuutatua mzozo huo wa Darfur.

Mjumbe huyo wa China alikuwa Darfur katika maadhimisho hayo akitoa misaada kuonesha jinsi nchi yake inavyounga mkono kusaidia juhudi hiyo.

Amesema nchi yake iko tayari kuongeza msaada wake katika eneo hilo.

Mapema wiki hii, Umoja wa Mataifa ulisema kwamba mashambulizi mapya, yamekuwa yakihatarisha maisha ya maelfu ya watu wa Darfur, huku raia kadhaa wakikimbia makazi yao, hali ambayo imefanya karibu watu milioni 2.2 kuyakimbia makazi yao kutokana na mzozo huo.

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, limearifu kuwa siku mbili za mashambulizi ya makombora na uvamizi uliofanywa na Jeshi la Sudan pamoja na wanamgambo wa Janjaweed, mapema mwezi huu katika eneo la magharibu mwa Darfur yalisababisha karibu wakimbizi elfu 12 kukimbilia mashariki mwa Chad.

Mashirika ya kimataifa yanakadiria kuwa watu laki mbili wameuawa tangu mwaka 2003, na wengine zaidi ya robo ya wakazi milioni sita wa Darfur kuyakimbia makazi yao.

Hata hivyo serikali ya Sudan inasema watu waliouawa ni elfu 9 tu.

Watu wapatao milioni 4.2 katoka eneo hilo wanaishi kwa kutegemea misaada.

Vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe, vinasemekana vilianza Februari 26 mwaka 2003 baada ya waasi kushambulia askari walinzi Darfur kaskazini, kwa madai ya tofauti za kiuchumi na kisiasa, ingawa ghasia nyingine za kikabila zilianza kufukuta mapema.

Serikali ya Sudan iliandikisha askari wapya na jeshi la wanamgambo linalojulikana kama Janjaweed, ambao wanasemekana kuhusika wazi katika mashambulio hayo ya Darfur.

Marekani imeelezea kuendelea kutoridhishwa kwake na kucheleweshwa kwa utawanyaji wa kikosi kipya cha Umoja wa Mataifa.

Serikali ya Sudan, imekuwa ikitaka kikosi kikosi cha kulinda amani kinachoundwa na Umoja wa Afrika tu, na kuonesha wazi kutotaka kikosi cha umoja wa mataifa.

Aidha Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Kulinda amani Jean-Marie Guehenno aliwahi kusema kuwa kukataa kwa Sudan kutakuwa na "madhara makubwa", kwa ajili ya kupeleka ujumbe kamilifu wa kikosi hicho cha kulinda amani cha umoja wa mataifa.

Kikosi chenye nguvu kilichopendekezwa cha Ujumbe wa Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa na Afrika huko Darfur chenye askari elfu 26,na 600, kilichoelezewa kama kikosi kikubwa zaidi cha kulinda amani duniani, bado hakijaanza kazi kutokana na kukosa askari na vifaa vya kijeshi.

Lakini ni askari elfu 9 na 200 tu kati ya hao waliopendekezwa ndio wameshapelekwa Darfur.