1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo kati ya Saudi Arabia na Iran wazidi makali

5 Januari 2016

Saudi Arabia inasema itarejesha upya uhusiano wa kidiplomasia , pale Teheran itakapoacha kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyengine. Riyadh wanasema wataendelea na juhudi za kusaka amani nchini Syria na Yemen

https://p.dw.com/p/1HY4z
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Saud Arabia,Adel al DjubeirPicha: Getty Images/AFP/A. Farwan

Saudi Arabia imevunja uhusiano na Iran ili kulalalamika dhidi ya kushambuliwa ofisi ya ubalozi wake mjini Teheran na waandamanaji waliokuwa wakilalamika dhidi ya kuuliwa Sheikh Nimr al Nimr,mshika bendera wa malalamiko ya waumini wa madhehebu ya shia katika nchi hiyo ya ufalme wa wahabi.

Viongozi wa Ryadh wametangaza kusitisha mawasiliano ya angani na uhusiano wa kibiashara pamoja na jamhuri ya kiislam ya Iran.

Akiombwa aelezee masharti gani yanahitajika ili kurejesha uhusiano kati ya nchi hizo mbili,balozi wa Saud Arabia katika Umoja wa Mataifa,Abdallah bin Yahya Al-Mouallimi amesema: "Sisi na Iran hatukuzaliwa tuwe maaduwi .Tabia ya serikali ya Iran ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyengine na hasa za kiarabu,ikiwa ni pamoja na nchi yetu ndio sababu ya kuchukua msimamo huu."

Juhudi za upatanishi zimeshika kasi

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Staffan de Mistura amepangiwa kuzitembelea Saud Arabia na Iran wiki hii kuhakikisha mvutano hauzidi makali kati ya nchi hizo mbili na kwa namna hiyo kuzidi kunyunyuzia mafuta katika cheche za moto za eneo hilo.

Iran Protest in Teheran gegen Hinrichtung in Saudi-Arabien
Maandamano mjini Teheran dhidi ya kunyongwa sheikh Nimr al Nimr nchini Saud ArabiaPicha: picture-alliance/AP Photo/V. Salemi

Mzozo wa Saud Arabia na Iran unafufua uhasama wa jadi kati ya nchi hizo mbili katika wakati ambapo vita vinapamba moto nchini Iraq,Syria na Yemen uhasama unaosababishwa na kiu cha kuania masilahi kati ya washiya na wasunni.

Saud Arabia inakamata nafasi muhimu katika juhudi za kuwaleta pamoja wanamgambo wa upinzani wanaoweza kushiriki katika mazungumzo ya amani pamoja na serikali ya rais Bashar al Assad wa Syria.

Umoja wa Mataifa ungependelea mazungumzo hayo ya amani yaanze january 25 ijayo mjini Geneva..

Marekani imeanza kuwasiliana na viongozi wa Ryadh na Teheran ili kuwasihi wavute subira-amesema hayo msemaji wa ikulu ya Marekani.

Die Linke wanataka biashara ya silaha isitishwe pamoja na Saud Arabia

Balozi wa Saud Arabia katika Umoja wa Mataifa Abdallah Bin Yahya Al- Mouallimi amesisitiza kuvunjwa uhusiano pamoja na Iran hakutoathiri juhudi za nchi yake za kusaka amani nchini Syria na Yemen.

Sahra Wagenknecht DIE LINKE
Kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto die Linke,Sahra WagenknechtPicha: picture-alliance/dpa/K.Nietfeld

Serikali kuu ya Ujerumani imezitolea wito serikali za Saud Arabia na Iran ziketi na kujadiliana.Msemaji wa serikali Steffen Seibert ameutaja uhusiano wa nchi hizo mbili kuwa na umuhimu mkubwa katika kupatiwa ufumbuzi mizozo ya Syria na Yemen.

Upande wa upinzani unaitaka serikali kuu isitishe ushirikiano wa aina pekee pamoja na Saud Arabia ili kuweza kuwa mpatanishi kati ya Iran na Saud Arabia.Kundi la chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto die Linke linakwenda umbali wa kutaka isitishwe biashara ya silaha kwa ncnhi hiyo ya kifalme.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters

Mhariri:Josephat Charo