1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo ndani ya AfD waongezeka

20 Aprili 2017

Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD cha nchini Ujerumani, kitafanya mkutano wake mkuu mwishoni mwa wiki hii, kwa lengo la kupata suluhu la mzozo wa madaraka uliopo.

https://p.dw.com/p/2baPC
Deutschland Pressekonferenz der AfD zu Medienordnung
Kiongozi mwenza wa AfD Frauke PetryPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Mzozo huo unatishia kuvunja azma yake ya kushinda viti kwa mara ya kwanza bungeni katika uchaguzi wa mwezi Septemba. Mkutano huo wa AfD unakuja wakati ambapo kiongozi mwenza wa chama hicho Frauke Petry, ametangaza kwamba hatokiongoza chama hicho kama mgombea mkuu wa nafasi ya kansela katika uchaguzi mkuu.

Mkutano huo wa siku mbili utakaoanza Jumamosi utawaleta wawakilishi wa chama hicho wasioelewana chini ya paa moja katika mji wa Cologne, na unatarajiwa kuzusha maandamano makubwa ya hadi watu 50,000 na ulinzi unatarajiwa kuwa mkali pia huku polisi wakitarajiwa kufikia 4,000.

Umaarufu wa AfD umedorora hadi chini ya asilimia kumi

Chama hicho kilikuwa kina umaarufu mkubwa wakati mmoja, hususan baada ya Ujerumani kukubalia idadi kubwa ya wakimbizi kuingia nchini mwake, lakini chama hicho kimeshuhudia umaarufu wake ukiporomoka katika chunguzi nyingi za maoni, kutoka umaarufu wa asilimia 15 miezi sita iliopita hadi chini ya asilimia 10 hivi sasa. Haya yote ni kutokana na mikwaruzano iliyopo baina ya wanachama wake.

Saarland Landtagswahlen Wahlplakate SPD  CDU
Mwanamke akitembea mbele ya mabango ya Kampeni ya uchaguzi UjerumaniPicha: Getty Images/S. Gallup

Na katika kile kinachoonekana kama kionjo tu cha joto litakalokuwa katika mkutano huo wa wikendi, kiongozi mwenza wa AfD Frauke Petry, alitangaza jana Jumatano kupitia ujumbe wa video katika mtandao wa kijamii wa Facebook kwamba, hatosimama kama mgombea mkuu katika uchaguzi mkuu wa Septemba huku akiwataka wanachama wa chama hicho wasioelewana wawe na sauti moja.

"Ili kutilia kikomo uvumi wote kuhusiana na suala hili, natumia fursa ya ujumbe huu wa video kusema wazi kwamba, sitosimama kama mgombea wala sitoshiriki uchaguzi huo," alisema Petry. "Ni muhimu kwangu kwamba tunaweza kujadiliana kuhusu masuala muhimu ya siku za mbeleni, ambayo yataamua msimamo wa chama cha AfD bila kuegemea uvumi katika miezi na miaka ijayo."

AfD hakiwezi kushinda kiti cha Kansela wa Ujerumani

Petry amehusika pakubwa katika mizozo ya ndani kwa ndani ya AfD, wakati ambapo amekuwa akijaribu kuonesha kwamba yeye ndiye mwenye msimamo wa kadri badala ya maafisa wengine wa chama hicho, ambapo kauli na misimamo yao ya wazi ya ubaguzi wa rangi imeshutumiwa pakubwa katika taifa zima.

Uamuzi wa Petry kutosimama kama mgombea mkuu wa chama katika uchaguzi mkuu, umeonekana kama ishara ya kujaribu kuhakikisha kwamba hatoshambuliwa na kuaibishwa katika mkutano huo ujao wa chama.

ENF Tagung in Koblenz
Frauke Petry akiwa pamoja na viongozi wengine akiwemo mgombea wa urais Ufaransa Marine Le PenPicha: Reuters/W.Rattay

Afd kimekuwa chama cha mrengo wa kulia kilicho na ufanisi mkubwa nchini Ujerumani baada ya vita vya pili vya dunia. Lakini hakiwezi kufananishwa na kile cha Marine Le Pen nchini Ufaransa kwani, hakina nafasi ya kushinda uchaguzi mkuu wa Ujerumani, ambapo Kansela Angela Merkel anasaka muhula wake wa nne baada ya takriban miaka 12 madarakani.

Lakini licha ya kuwa vyama vyote vimeondoa uwezekano wa kufanya kazi na AfD, huenda chama hicho kikapata kura za kutosha na kupelekea hesabu ya kuunda serikali ya muungano kuwa ngumu zaidi.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE

Mhariri: Iddi Ssessanga