1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Chakula Afrika ya Magharibi

P.Martin25 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CSsz

Ghasia zilizozuka hivi karibuni katika nchi kadhaa za Afrika Magharibi kuhusika na kuongezeka kwa bei za vyakula,ni ishara mpya ya matatizo yanayolikabili Bara Afrika.Takriban nusu ya watu katika bara hilo,huishi kwa kutumia Dola moja kwa siku. Baada ya Mauritania na Morocco,juma lililopita Senegal nayo ilishuhudia maandamano ya ghasia kupinga bei za vyakula zinazoendelea kuongezeka.Takriban kila nchi barani Afrika, imeathirika kwa tatizo hilo,lakini bila ya kushuhudia machafuko kama ilivyotokea Afrika ya Magharibi eneo lenye idadi kubwa ya nchi zilizo masikini kabisa duniani.

Hata hivyo,Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa-FAO bwana Jacques Diouf ameonya juu ya hatari ya kuzuka machafuko ya kijamii na kisiasa katika nchi zinazoendelea kwa sababu ya kuzidi kuongezeka kwa bei za nafaka kote duniani.Kwa mujibu wa FAO,hivi sasa ni vigumu kudhibiti bei hizo na mataifa yatakayoathirika vibaya zaidi ni yale ambayo huagizia vyakula nchi za ngámbo.Inatathiminiwa kuwa bei hizo zitabakia juu kwa angalao miaka 10 ijayo.Kwa hivyo mataifa yanayonunua vyakula nchi za nje,hayana budi isipokuwa kubadili tabia za mlo na kuanza kutumia vyakula vya kienyeji.

Lakini hata hapo kuna tatizo,kwani mabadiliko ya hali ya hewa yanahatarisha kilimo barani Afrika, ambako hali ya ujangwa inaongezeka;na mara nyingi bara hilo hukabiliwa na mchanganyiko wa ukame na mafuriko.Mabadiliko ya hali ya hewa barani Afrika,humaanisha kuwa katika miaka 12 ijayo, mavuno yatapunguka kwa nusu katika nchi zinazotegemea mvua kuendesha kilimo chake.Hayo alieleza mkuu wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa-WFP Bibi Josette Sheeran,wakati wa ziara yake ya hivi karibuni katika Afrika ya Magharibi. Akaongezea kuwa bei za vyakula zimeongezeka kwa asilimia 50 katika kipindi cha miaka 5 iliyopita na wakati huo huo,idadi ya watu wasio na uwezo wa kupata chakula cha kutosha,imeongezeka.Kwa maoni ya Sheeran,mabadiliko ya hali ya hewa,kupanda kwa bei za vyakula pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watu ni mambo yanayoweza kusababisha mripuko barani Afrika.

Kuambatana na WFP,nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo,asilimia 75 ya umma wa milioni 60 hauna chakula cha kutosha na watu milioni 1.5 wanakabiliana na njaa.Kuanzia Ivory Coast katika Afrika ya Magharibi hadi Zimbabwe,kusini mwa Afrika,ambako mfumuko wa bei unapiga fora kote duniani,familia hazina njia nyingine isipokuwa kupunguza idadi ya milo yake.