1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Gaza. Umoja wa Ulaya kushika usukani katika mpango wa amani.

Eric Kalume Ponda26 Januari 2009

Juhudi za kutafua amani ya kudumu katika eneo la mashariki ya kati zimeimarishwa huku hali ya utulivu ikiendelea.

https://p.dw.com/p/GgP8
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaokutana Brussels.Picha: picture-alliance / dpa

Baada ya kumalizika kwa muda wa wiki moja uliotangazwa na Israel na chama cha Hamas wa kukomesha vita katika eneo hilo hakuna milio na makombora au mabomu iliyosikika katika eneo hilo.


Hali hiyo imetokea huku Israel ikijiandaa kuwatetea wanajeshi wake kutokana na uwezekano wa kushtakiwa kwa uhalifu wa kivita wakati wa vita hivyo vilivyodumu kwa muda wa siku 22 katika eneo la Gaza.


Shutuma kali zinazoendelea kutolewa dhidi ya wanajeshi wa Israel kwamba walikiuka sheria za kimataifa wakati walipovamia eneo la Gaza, sasa zimeiweka Israel katika hali ya tahadhari kubwa.


Hivyo waziri mkuu wa nchi hiyo Ehud Olmert amewahakikishia wanajeshi wake kwamba kila jitihada za kisheria zitachukuliwa kuwalinda wanajeshi hao dhidi ya kufikishwa katika mahakama ya kimataifa.



Wanajeshi wa Israel wanashtumiwa kwa kutumia mabomu ya kemikali ya Fosiforasi na kuwazuia raia wasitoroke maeneo ya mapigano mbali na madai ya kutumia nguvu za kijeshi kupita kiasi wakati wa vita hivyo.


Hatua hiyo imetokea huku mashauri ya kutafuta amani ya kudumu yakiendelea mjini Cairo ambako kundi la wajumbe wa chama cha Hamas walikutana na mpatanishi mkuu kwenye mpango huo unaoongozwa na Misri Omar Suleiman.


Wajumbe hao walisema kuwa wako tayari kufikia mkataba wa kukomesha mapigano kwa muda wa mwaka mmoja iwapo Israel itafungua maeneo yote ya mpkani na kuondoka kabisa katika eneo la Gaza.


Misri ilifunga eneo la mpakani la Rafah baada ya kumalizika kwa muda uliotangazwa na Israel kwa kuhofia kwamba huenda wanajeshi wa Israel wangelishambulia eneo hilo kuharibu mahandaki ambayo inasema yanatumiwa kuingizia Silaha ukanda wa Gaza.


Mawaziri wa mambo ya nchi za nje kutoka umoja wa Ulaya wanaokutana mjini Brussel wametoa wito wa kudumishwa kwa mshikamano wa Wapalestina ili amani ya kudumu iweze kupatikana katika eneo hilo la mashariki ya kati.


Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Sweden Carl Bidt amesema kuwa sasa amani ya eneo hilo lsa mashariki ya kati haiwezi kupatikana hadi pale kutakapokuwa na usawea baina ya Israel na Hamas. Carl Bildt alisema `` Kitu cha msingi ni kufungua njia ya kuingia Gaza, ili raia wa Gaza wawe na haki sio tu ya kukidhi mahitaji yao bali pia kuishi. Na bila kuwapa nafasi hiyo ya kuishi vizuri kuna kitisho cha kujihusisha na vitendo viovu na hali ya kukata tamaa´´


Mashariano hayo pia yanakusudiwa kutafuta njia bora ya kufunguliwa kwa maeneo yote ya mpakani ili kutoa nafasi ya kuingizwa kwa misaada ya binadamu katika eneo la Gaza.


pia akizungumza wakati wa kikao hicho waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza David Milband alisikitishwa na mgawanyiko uliopo miongoni mwa Wapalestina wenyewe. David Milband alisema`` Mzozo wa hivi punde katika eneo la mashariki ya kati ni dhihirisho la kushindwa kwa siasa za eneo hilo na Umoja wa Ulaya unataka kushika usukani kuufufua mpango wa kuwa na dola mbili katika mashariki ya kati´´


Wakati huo huo waziri wa maongozi ya mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya Javieer Solana anatarajiwa kuwasili katika eneo hilo la mashariki ya kati kwa ziara itakayomchukua katika mataifa 4 kutoa msukumo zaidi wa mpango wa amani katika kanda hiyo. Javier Solana anatarajiwa kuwa na mazungumzo na maafisa wa serikali ya Israel, Palestina, Misri na Jordan.


Israel ilitangaza kusimamisha mapigano kwa muda wa wiki moja ingawa ilionya kuwa haitasita kujibu mashambulio yoyote ya maroketi yatakayofanywa na Hamas.