1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chanzo cha mzozo baina ya nchi hizo ni pamoja na mafuta

14 Novemba 2017

Uhusiano baina ya taifa kubwa la Mashariki ya kati, Saudi Arabia na Iran,  kwa miongo mingi umekuwa wa wasiwasi kutokana na nchi hizo kuzozana kuhusu masuala matatu- mafuta, dini na utawala

https://p.dw.com/p/2nbEr
Iran Ayatollah Ali Khamenei, Oberster Religionsführer | Gespräch mit Studenten
Kiongozi wa kidini wa Iran, Ali Khamenei.Picha: Reuters/Leader.ir

Kila mmoja anajinasibu kuwa mtetezi wa  madhehebu mawili makuu ya dini ya kiislamu. Saudi Arabia, inatetea dhehebu la Sunni na Iran ipo upande wa Shia.

 Hayo yanajiri wakati mvutano huo ukiongezeka wiki hii, baada ya Riyadh kuituhumu Tehran kwa  kufanya uvamizi wa kijeshi wa moja kwa moja unaohusishwa na vita vya Yemen.

 Sababu kuu za mivutano hiyo

Mwaka 1973 wakati wa vita vya Arab-Israel, taasisi ya usafirishaji wa mafuta(OPEC) iliongeza bei ya mafuta.

Wazalishaji wa mafuta kutoka Arabuni, walitoa amri ya kuzipiga marufuku nchi ambazo zinatajwa kuipa ushirikiano Israel, ikiwamo Marekani.

Mzozo unaongezeka

 Iran ilitaka bei kubwa zaidi ya mafuta ghafi ili kupata fedha za kuendeleza mpango wake wa maendeleo ya viwanda, wakati huo, Saudi arabia  ilitaka  kuzuia ongezeko hilo kubwa  la bei ya mafuta ili kuwasaidia washirika wake,  Marekani.

Jamhuri ya kiislamu ya Iran, ilianzishwa Aprili 1979 baada ya mapinduzi yaliyouondoa utawala wa kifalme ulioelemea nchi za magharibi. mataifa  ya Kisunni katikakanda hiyo yakaishutumu  Iran kuwa inataka kusafirisha mapinduzi yake katika nchi hizo.

Mnamo Septemba 1980, Iraq iliivamia Iran na kusababisha vita vilivyodumu kwa miaka nane. Saudi Arabia, iliisaidia kifedha serikali ya Iraq dhidi ya Iran, na kuzishawishi nchini nyingine zenye waumini wengi wa madhehebu ya  Sunni, kufanya hivyo hivyo.

Askari wa usalama wa Saudi waliyakandamiza maandamayo dhidi ya Marekani  mjini Mecca Julai 1987yaliyofanywa na mahujaji kutoka Iran. Zaidi ya watu 400 wengi wakiwa raia wa Iran, waliuawa.

Raia wa Iran wenye hasira waliuvamia na kupora mali katika ubalozi wa  Saudi, mjini Tehran, na Aprili 1988,  Saudi Arabia ikavunja uhusiano wa kibalozi  na Iran.

Kuchaguliwa  mwanamageuzi wa Iran, Rais Mohammed Khatami, mnamo Mei 1997, kulichangia kuimarishwa kwa mahusiano na Saudi Arabia  ambapo Mei 1999, Rais huyo alifanya  ziara ya kihistoria nchini humo.

 Lakini uvamizi wa Iraq, ulioongozwa na Marekani mwaka 2003, ulizusha mzozo mpya kwa kukiondoa chama Baath,  kilichokuwa kikitawala na kuruhusu Washia kuongoza. Hatua hiyo  ilisababisha Iraq kuwa chini ya nyanja ya ushawishi wa Iran. 

Wakati maandamano yakichipuka katika nchi za Mashariki ya Kati mwaka 2011,  Riyadh iliyatuma majeshi yake kwa nchi jirani ya Bahrain ambako kuliibuka waandamanaji, wengi wakiwa ni wa dhehebu la Shia. 

Riyadh  iliishutumu Tehran kwa kuchagiza  mzozo  huo katika visiwa vinavotawaliwa na  Wasuni.

Mahasimu hao walijiandaa tena kwa mapigano mapya,  mwaka 2012, wakati mzozo wa Syria ulipozuka.

Iran ilimsaidia Rais Bashar al-Assad kwa kumpa vikosi vya kijeshi na fedha ili kupambana na waasi wa Suni.

Baadaye, Saudi Arabia iliwasaidia waasi, lakini ikajiunga na muungano unaoongozwa na Marekani, katika kupambana  na makundi ya Wasuni wa kiislamu yenye msimamo mkali.

Kadhalika, Saudi Arabia na Iran, waliupinga mgogoro wa Yemen. Machi 2015 Riyadh iliunda muungano wa waarabu wa Sunni,  ili kuingilia ushirikiano wa rais wa Yemen, wakati Tehran ikiwasaidia wanamgambo wa Huthi wa dhehebu la Shia.

Mnamo Septemba 2015, mahujaji zaidi ya 2300 wakiwamo mamia ya Wairan, walipoteza maisha kutokana na kukanyagana wakati wa kutekeleza ibada ya hija.

Baada ya tukio hilo, kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, alisema familia inayotawala ya  Saudi, haina sifa ya kusimamia maeneo matakatifu ya Kiislamu.

Saudi-Arabien Riad König Salman und Saad Hariri Ex-Premierminister Libanon
Mfalme wa Saudi Arabia, Salman akiwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon, Saad Hariri hivi karibuni. Picha: picture-alliance/AA/Bandar Algaloud

Mnamo Januari 2016, Saudi Arabia, ilimnyonga kiongozi  maarufu wa madhehebu la Washia, Nimr al-Nimr kwa kosa la ugaidi, akitajwa kuwa chanzo cha waandamanaji wanaoipinga serikali .

 Iran ilichukizwa. Mipango ya kidiplomasia iliyofanywa na Saudi nchini Iran,  ilivamiwa na waandamanaji na hivyo Riyadh ikavunja uhusiano wake tena na Iran

Kadhalika wanamgambo wenye nguvu wa Hezbollah; wa madhehebu ya Shia nchini Lebanon, ambao ni washirika wa Iran, walitajwa kama magaidi, mnamo Machi 2016 na ghuba ya falme za kiarabu.

Hayo yote yalitokea baada ya  kiongozi wake, kuishutumu Saudi Arabia kwa kutaka kuchochea ´uasi´kati ya Waislamu wa madhehebu ya Suni na Shia

 Wakati hayo yakijiri, Novemba 2017, Waziri Mkuu wa  Lebanon, Saad Hariri, alitangaza kujiuzulu akiwa Riyadh,  akitaja kuwa kuna njama zinazofanywa na Iran, nchini humo dhidi ya usalama wake, kupitia kundi la Hezbollah.

 Mnamo Juni 2017, Saudi Arabia, na washirika wake, walivunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Qatar, wakiishutumu kwa kukuza ukaribu wake na Iran huku  wakiunga mkono makundi ya itikadi kali.

Baadaye, Oktoba 2017, Saudi Arabia, ilisema inamuunga mkono Rais wa Marekani, Donald Trump,  katika mikakati yake  madhubuti dhidi ya Iran baada ya kukataa kuthibitisha makubaliano juu ya mpango wa nyuklia wa wa Iran  yaliofikiwa 2015 kati ya Iran na madola sita yenye nguvu duniani.

 Mwandishi: Florence Majani(UTC)

 Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman.