1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Korea: Kaskazini yafanya mazoezi ya kijeshi.

Admin.WagnerD26 Novemba 2010

Siku ya tatu sasa na mzozo katika eneo la Korea hauonekani kutulia. Korea Kaskazini leo imefanya mazoezi ya kijeshi karibu na mpaka na jirani yake, Korea Kusini.

https://p.dw.com/p/QIt2
Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong IlPicha: AP

Na si hayo tu, utawala huo wa Kikomunisti umeonya kuwa luteka ya pamoja ya Marekani na Korea Kusini iliyopangwa kufanyika mwishoni mwa juma hili ni kama kauli mbiu ya vita katika eneo hilo la Korea.

Kisiwa cha Yeonpyeong huko Korea Kusini kiliamkia milio ya risasi na mizinga na raia ilibidi kukimbilia usalama wao, kwani milio hiyo iliwakumbusha asubuhi ya Jumanne pale mizinga ya Korea Kaskazini ilipoangukia kisiwa hicho na kuwaua watu wanne, kuwajeruhi wengine 18 na kuteketeza nyumba kadhaa kisiwani humo.

NO FLASH nordkoreanischen Beschuss der südkoreanischen Insel Yonpyong
Kisiwa cha Yeonpyeong, Korea Kusini, kikiwaka moto.Picha: AP

Hata hivyo, utawala wa Korea Kusini uliondoa wasiwasi kuwa milio hiyo ya mizinga ilikuwa ni jirani yake Korea Kaskazini wakifanya mazoezi ya kijeshi, na kwamba hakuna makombora au mizinga iliyoangukia ardhi ya Kusini.

Hali hii inakuja wakati serikali ya Lee Myung -bak inakabiliwa na changamoto za ndani baada ya Waziri wa ulinzi kujiuzulu jana kutokana na shutuma kuwa Korea Kusini haikuwa na jibu la haraka dhidi ya uchokozi wa jirani yake wa Kaskazini.

Haiti Erdbeben Flughafen Port-au-prince
Ndege za kivita za MarekaniPicha: AP

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi aliliambia shirika la habari la AFP kuwa miripuko ilisikika kati ya saa sita mchana na saa tisa- saa za huko Korea na ilionekana kwamba miripuko hiyo ilitokea Korea Kaskazini.

Kulingana na kituo kimoja cha Televisheni walinukuu vyanzo vya habari kutoka jeshini vilivyosema kulikuwa na kiasi ya miripuko 20 hivi, lakini haikuangukia ardhi ya Korea Kusini.

Waandishi wa habari waliokuwa katika kisiwa cha Yeonpyeong, waliripoti kuwa watu walikuwa mbioni kujinusuru waliposikia miripuko hiyo. Jumanne wiki hii Korea Kaskazini ilirusha mizinga katika kisiwa hicho na kuwaua watu wanne, wakiwemo wanajeshi wawili wa Korea Kusini. Watu wengine 18 walijeruhiwa na nyumba kadhaa kuteketezwa moto.

Manowari ya iliyobeba ndege za kivita za Marekani nayo ikiwa njiani kuelekea katika bahari ya Manjano, tayari kwa ile luteka ya pamoja na Korea Kusini iliyopangwa kufanyika jumapili. Hili halijakosa kuwakera Wakorea Kaskazini ambao wameitaja luteka hiyo ya pamoja kama firimbi ya kuanzisha vita katika eneo la Korea. Iwapo ilikuwa imepangwa tokea kitambo au la- kufanyika kwa Lteka hiyo pia huenda ni ishara kwa Korea Kaskazini kuwa washirika wa jirani yake Kusini- watasimama na Seoul kuzuia kiburi na uchokozi wowote kutoka PyongYang.

Mwandishi: Munira Muhammad/AFPE

Mhariri: Othman Miraji.