1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa serekali katika Uturuki

Güngör,Baha4 Julai 2008

Kengele za kuonya hatari ya kuweko mzozo wa siasa ndani huko Uturuki zinagonga vikali hivi sasa.

https://p.dw.com/p/EWRM
Waziri mkuu wa Uturuki, Tayyip ErdoganPicha: AP

Chama tawala chenye kuelemea siasa za asilia za Kiislamu,AKP, kinatishiwa kupigwa marufuku kupitia mahakama ya kikatiba, na waziri mkuu, Recep Tayyip Erdogan, naye huenda akapigwa marufuku asijishughulishe na siasa. Kujibu hayo, yeye sasa ameamrisha wakamatwe wapinzani wa serekali yake, akiwashuku wamefanya mashambulio na wamepanga njama za kutaka kufanya mapinduzi. Haya yote yamezidisha mkwaruzano katika hali ambayo tangu hapo ilikuwa ya mvutano. Hii ni kwa mujibu wa Baha Güngör, mkuu wa idara ya lugha ya Kituruki hapa Deutsche Welle.

Wakiwa na wasiwasi, wananchi wa Ulaya siku hizi wanaiangalia Uturuki. Suluhisho la mzozo uliodumu kwa miaka baina ya chama cha Ki-Conservative kilicho na muelekeo wa kidini, AKP, na watu wenye kutaka ubakie mtengano baina ya dola na dini hauonekani. Hamna upande wowote unaotaka kurejea hatua hata moja nyuma ya msimamo wake.

Hali hiyo imetokana na kama ifuatavyo: Huenda hata mwezi huu mahakama ya kikatiba ikaamua kama chama cha AKP kipigwe marufuku. Hiyo itamaanisha kwamba waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan pamoja na karibu wanasiasa wengine 40 wataweza kupigwa marufuku kujishughulisha zaidi na siasa. Sababu ya hukumu hiyo itatajwa kwamba Chama cha AKP kimekuwa kituo cha harakati za siasa kali za kidini kupingana na msingi wa utawala wa Jamhuri ya Uturuki unaotaka siasa na dini visichanganyishwe. Kutokana na sababu hiyo, tayari hapo kabla vyama vinne vya Kiislamu vilipigwa marufuku, vyote vikuwa chini ya kiongozi na mlezi wa kisiasa wa Erdogan, waziri mkuu wa zamani na kiongozi wa Kiislamu. Necmettin Erbakan.

Kwa hivyo, serekali imewakamata madarzeni ya watu wanaoshukiwa ni wanachama wa jumuiya ya chini kwa chini ilio na jina la Ergenekon. Jina hilo linaelezea nchi ya kale ya watu wenye asili ya Kituruki. Kwa mujibu wa hadithi, watu wa nchi hiyo walipata hasara kubwa katika vita dhidi ya maadui wao, na baadae walijikusanya kama kikundi kidogo. Baada ya vizazi kupita, waliongezeka kwa idadi na kuchipuka katika maeneo mbali mbali ya dunia.

Ishara hiyo haijakosewa. Wapinzani wa serekali ya sasa, ambao ni watu wanaotaka dola na dini zitenganishwe, kama vile alivoshikilia muasisi wa dola ya kisasa ya Uturuki, Kemal Atatürk, wanajihisi wametengwa, kisiasa, baada ya uchaguzi mkuu uliofanywa mwaka mmoja uliopita. Chama cha AKP, kikiwa na wingi usiokuwa na wasiwasi bungeni, tangu wakati huo kinaweza kuwasha na kuzima, kama kinavotaka. Kitaweza tu kuzuiliwa na mahakama ya kikatiba ambayo kwamba wapinzani na wafuasi wa kindakindaki wa Atatürk mara nyingi walifaulu pale wanapoita isikilize mashtaka yao.

Kutokana na msukumo wa kutoka Ulaya, Tayyip Erdogan anafanya makosa ya kijifikiria kwamba yeye hafanyi makosa. Zile ahadi kubwa kubwa alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi, kama vile kuondosha amri ya kupiga marufuku wanawake kuvaaa ushungi katika vyuo vikuu pamoja na kuchukuwa hatua zaidi za kulazimisha nchi hiyo iwe ya Kiislamu zaidi -yote hayo aliyafanya kuwatuliza wananchi wa kawaida. Erdogan aliyafanya yote hayo bila ya kuangalia hasara zilizotokea, na, kwa sehemu, alitumia nguvu ili kufikia malengo yake. Hataki suluhisho na huchochea kuweko hali ya kupimana nguvu na wapinzani wake.

Kabla ya kumalizika mapambano haya ya kupimana nguvu, tusitarajie mwisho wa mzozo huu wa siasa za ndani za Uturuki. Upande utakaoshinda baadae utabeba dhamana ya kuielekeza Uturuki katika njia ya kuingia kwenye Umoja wa Ulaya. Lakini nchi za Magharibi haziwezi kumudu kuwa na Jamhuri ya Uturuki yenye thamani za Kiislamu zilizovuka mipaka au Uturuki iliojengeka kwa misingi ya thamani za uzalendo uliopindukia. Uwezekano wa kutokea michafuko ndani nchini humo utaleta hatari ya kupoteza mshirika wa kisiasa na wa kijeshi anayeaminika barani Ulaya. Mshirika huyo anatakiwa kwa haraka hivi sasa na Ulaya, kwa vile kuna maeneo ya mizozo iliojaa michafuko, na ambayo ni jirani na Uturuki. Kuyavunja mashauriano ya kutaka kuiingiza Uturuki katika Umoja wa Ulaya, kama vile wanavohoji wale wanaopinga Uturuki kuingizwa katika umoja huo, kutatoa ishara mbaya sana. Hatua hiyo itazitia moyo pande mbili zinazobishana vikali nchini humo kun'gan'gania kwa ukali misimamo yao.