1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Srilanka

Oumilkher Hamidou23 Aprili 2009

Baraza la usalama lawalaani waasi wa LTTE

https://p.dw.com/p/HcVP
Rais wayapa kisogo mapigano SrilankaPicha: AP

Waasi wa Tamil Eelam,-LTTE,wanaendelea kukabiliana na vikosi vya jeshi la serikali ya Srilanka,vinavyowazingira,licha ya mwito wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa wa kuwataka waweke chini silaha.

Maelfu ya raia wanajikuta kati kati ya mapigano kati ya jeshi la Srilanka na waasi hao wa Tamil Eelam.Kwa mujibu wa jeshi waasi hao wanadhibiti eneo la kilomita 10 hadi 12 tuu za mraba.

"Mapigano yanaendelea hapa na pale,lakini la muhimu kwetu ni kuwahamisha raia" amesema hayo msemaji wa jeshi jenerali Udaya Nanayakkara,aliyeongeza tunamnukuu"Tutawashinda nguvu waasi mara tuu tutakapokamilisha kuwahamisha raia."Mwisho wa kumnukuu.

Jana baraza la usalama la Umoja wa mataifa liliwataka waasi hao wa LTTE waweke chini silaha,wasalim amri na kuwaachia huru raia wanaowashikilia mateka.

Mwenyekiti wa baraza la Usalama la Umoja wa mataifa,balozi wa Mexico Claude Heller anasema:

"Wanachama wa baraza la usalama wanalilaani vikali kundi la kigaidi la LTTE kwa kuwatumia raia kama ngao na kuwazuwia kulihama eneo la mzozo.Kwa namna hiyo wanachama wa baraza la usalama wanawataka waasi wa LTTE waweke chini haraka silaha na kuachana na ugaidi."

Baraza la usalama la Umoja wa mataifa limezitolea mwito pande zote,ikiwa ni pamoja na serikali ya Srilanka ziheshimu sheria za kimataifa kuhusu hifadhi ya raia na kuwaruhusu watumishi wa mashirika ya kiutu waingie katika maeneo ya mapigano.

Baraza la usalama limewataka waasi wa LTTE warejee katika meza ya mazungumzo kusaka ufumbuzi wa amani kwa mzozo wa jimbo hilo.

Mkutano huo wa dharura wa baraza la usalama umeitishwa ili kusikiliza ripoti ya mjumbe maalum wa katibu mkuu Ban Ki-Moon,Vijay Nambiar kuhusu hali namna ilivyo katika eneo la mapigano nchini Srilanka.

Wakati huo huo rais Mahinda Rajapakse wa Srilanka ameondowa uwezekano wa kumsamehe mkuu wa waasi Vellupillai Prabhakaran.

Baada ya miaka 37 ya mapambano ya kutaka kujitenga,wakuu wawili wa waasi wa Tamil wamejisalimisha kwa jeshi la serikali jana katika wakati ambapo walimwengu wamezidi kuingiwa na hofu kutokana na milolongo ya raia wanaoyapa kisogo mapigano.


Mwandishi Hamidou Oummilkhheir

Mhariri Abdul Rahman