1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Syria wachacha

2 Mei 2013

Majeshi ya Syria yamezidisha mashambulio dhidi ya waasi katika mji wa Homs yakisaidiwa na wataalam wa kivita kutoka Iran na kikundi cha Hezbollah kutoka Lebanon

https://p.dw.com/p/18QUc
Mgogoro wa Syria
Mgogoro wa SyriaPicha: Reuters

Shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria limesema majeshi ya Assad yamekuwa yakipata udhibiti wa maeneo mengi katika mji wa Homs ambao umetajwa kuwa kitovu cha uasi dhidi ya utawala wa rais Bashar al Assad. Shirika hilo limesema pia kuwa zaidi ya familia 800 zimejipata katika njia panda kwa mwaka mzima zikikosa namna ya kutoroka huku mamia wengine wakijeruhiwa.

Kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah
Kiongozi wa Hezbollah Hassan NasrallahPicha: Joseph Eid/AFP/Getty Images

Aidha shirika hilo limesema kuwa kudhibitiwa kwa mji huo wa kale wa Homs na majeshi ya Assad,kutasababisha mapigano ya kimadhehebu kwani wengi wa wakaazi wa mji huo ni wasunni.Homs imegawika kwa misingi ya kidini na kimadhehebu ikiwa na waislamu wa Kisunni, na kialawi, wakristo na watu wa dini nyinginezo. Mkuu wa shirika hilo la kuchunguza haki za binadamau Rami Abdel Rahman amesema maafisa kutoka Iran na kundi la wanamgambo la Hezbollah kutoka Lebanon wamekuwa wakiongoza operesheni za kijeshi katika mji wa Homs ambao ni ngome ya waasi.

Hezbollah yakiri kushiriki katika vita Syria

Hezbollah tayari imeshasema kuwa wanachama wa kundi lao wamekuwa wakipigana katika eneo la Qusayr katika jimbo hilo la Homs.Mwezi uliopita Rais Assad alisema utawala wake hauwezi kushindwa katika vita hivyo akidai kushindwa kutakuwa mwisho wa Syria na kuongeza kuwa hadhani kama watu wa Syria watakubali hali hiyo kutokea.

Huku shinikizo likizidi kwa Rais wa Marekani Barrack Obama kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya utawala wa Syria kutokana na shutuma za matumzi ya silaha za kemikali,kura ya maoni iliyofanywa na shirika la habari la Reuters na kampuni ya utafiti ya Ipsos zimeonyesha kuwa wamarekani wengi hawataki nchi yao iingilie kati katika mzozo wa Syria hata kama silaha hizo zilitumika.

Wamarekani wengi wanapinga nchi yao kuingilia

Ni asilimia 10 tu ya wamarekani waliohojiwa katika kura hiyo ya maoni ambao wanahisi Marekani inapaswa kujihusisha katika vita hivyo huku asilimia 61 wakipinga.Afisa wa shirika la Ipsos Julia Clark amesema wengi wa raia wa Mareakni wanahisi hakuna haja baada ya vita vya Afghanistan na vya Iraq ambavyo Marekani ilituma majeshi yake.Utafiti huo ulibaini kuwa asilimia 36 ya wamarekani hawajawahi kusikia au kusoma kuhusu vita vya Syria.

Rais wa Marekani Barack Obama
Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: Getty Images

Vita hivyo vya Syria vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 70,000 na zaidi ya wakimbizi milioni 1.2 wameikimbia nchi hiyo tangu vianze mwaka 2011 lakini Rais Obama amekuwa akijiepusha na mjadala wa taifa lake kuchukua hatua za kijeshi licha ya kutangaza mwaka jana kuwa iwapo utawala wa Assad utatumia silaha za kemikali basi itamlazimu kubadilisha mtazamo wa serikali yake.Lakini mapema wiki hii Obama ameonekana kuwa muangalifu zaidi kuhusiana na hilo akisema Marekani inahitaji kuwa makini zaidi na sio kukimbilia kuchukua hatua bila ushahidi wa kutosha.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/Afp
Mhariri: Daniel Gakuba.