1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa pande nne mjini Berlin

21 Januari 2015

Wanajeshi wa Ukraine wamefyetuliana mizinga na waasi mashariki ya Ukraine.Serikali ya mjini Kiev inadai wanajeshi wa Urusi walishiriki katika mapigano hayo na kwa namna hiyo kuzidisha makali ya mzozo huo,

https://p.dw.com/p/1EOWq
Wanajeshi wa UkrainePicha: picture alliance/AA

Kuzidi makali mzozo huo,baada ya wiki kadhaa za utulivu ni tukio sambamba na malumbano yanayoendelea kwa mbali kati ya Moscow na Washington.

Alikuwa Barack Obama aliyesema katika hotuba yake kwa taifa,"madola makuu hayawezi kuyaonea madogo na kwamba Urusi imetengwa zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote mwengine huku uchumi wake ukilega lega."Moscow imejibu na kuituhumu Marekani kutaka kuudhibiti ulimwengu.Ikulu ya rais nchini Urusi-Kremlin imeituhumu pia Washington kuutumia mzozo wa Ukraine ili kutaka "kuzikaba shughuli za kiuchumi za Urusi na kumpindua Vladimir Putin."

Vikosi vya Urusi katika mapigano ya Luhansk

Baada ya siku kumi za kuzidi makali mapigano pamoja na waasi,Kiev imelilaumu jeshi la Urusi kuwashambulia wanajeshi wake katika jimbo la Luhansk.Tuhuma hizo kali ni za kwanza za aina yake tangu makubaliano ya Minsk, septemba mwaka jana, yaliyopelekea silaha kuwekwa chini, licha ya makubaliano hayo kuvunjwa mara kwa mara. Jibu la Urusi halijakawia kutolewa.Waziri wa mambo ya nchi za nje Sergei Lavrow anajibu tuhuma hizo kwa kusema "ushahidi uko wapi"?

Davos WEF Auftritt Poroschenko 21.01.2015
Rais Poroschenko akihutubia kongmano la kiuchumi DavosPicha: Reuters/R. Sprich

Kutokana na hali namna ilivyo, rais Petro Poroschenko wa Ukraine ameamua kufupisha ziara yake katika kongamano la kimataifa la kiuchumi huko Davos na kurejea nyumbani.

Katika jimbo la Luhansk lililojitenga pamoja na lile la Donetsk mwezi wa April mwaka jana, vikosi vya serikali vimebanwa katika kila pembe.Katika uwanja wa ndege wa Donetsk,mapigano yamepamba moto,siku chache baada ya jeshi la serikali kuwarejesha nyuma waasi.

Kama hali namna ilivyo kwengineko katika jimbo hilo,mizinga inaendelea kufyetuliwa Donetsk na kuangamiza maisha ya raia wasiopungua watano na wengine 29 kujeruhiwa usiku wa jana kuamkia leo.

Matumaini mazungumzo ya Berlin yataleta tija

Kutokana na hali namna ilivyo mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Ukraine, Urusi, Ujerumani na Ufarana watakutana mjini Berlin kwa lengo la "kuzuwia mapigano yasizidi makali na kuzuwia kitisho cha mvutano kati ya Moscow na Kiev.

Ukraine Donezk Krankenhaus Raketenangriff 19.01.2015
Hospitali yasham,buliwa kwa mizinga DonetskPicha: picture-alliance/dpa/M. Parhomenko

Kansela Angela Merkel amesema anataraji mkutano huo wa pande nne utasaidia kutuliza hali ya mambo mashariki ya Ukraine.Akizungumza na waandishi habari mwishoni mwa mazungumzo yake pamoja na rais wa Azerbaidjan Ilham Alyev,kansela Angela Merkel amesema tunanukuu""Hatutaki kikao chengine cha mazungumzo kati ya marais na ambacho hakitaleta tija yoyote."Mwisho wa kumnukuu.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga