1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Ukraine wazidi Makali

21 Machi 2014

Ukraine imetia saini vifungu vya kisiasa vya mkataba vya ushirikiano katika mkutano wa viongozi wa Umoja huo mjini Brussels huku mgogoro wa Crimea ukizidi kupalilia mvutano kati ya Moscow na nchi za magharibi.

https://p.dw.com/p/1BTjo
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akikutana na waziri mkuu Jazenjuk wa Ukraine mjini BrusselsPicha: picture-alliance/dpa

Kwa namna hiyo Umoja wa Ulaya unabainisha uungaji mkono thabiti kwa Ukraine inayowakilishwa mkutanoni na waziri mkuu Arseniy Yatsenyuk.

"Kutiwa saini vifungu vya kisiasa vya mkataba wa ushirikiano ni "thibitisho kamili la mshikamano pamoja na Ukraine" amesema rais wa Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy na kuongeza tunanukuu" mkataba huo utawapatia wananchi wa Ukraine matumaini ya hali bora ya maisha wanayoistahiki." Mwisho wa kumnukuu

Wakati huo huo Umoja wa ulaya unafungua njia ya kuondowa ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazoagiziwa kutoka Ukraine ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuinua shughuli zinazozorota za kiuchumi. Brussels pia inazingatia uwezekano wa kuipatia Ukraine msaada wa kiuchumi wenye thamani ya Euro bilioni 11.

Umoja wa Ulaya waionya Urusi

Wakati wanainyooshea mkono Ukraine,viongozi wa Umoja wa ulaya wanaokutana mjini Brussels wanazidisha shinikizo kwa Urusi kufuatia uamuzi wake wa kuimeza Crimea.Jana viongozi hao wameongeza marufuku ya safari na kuzuwiliwa milki za maafisa wa serikali za Urusi na Ukraine na kufikia watu 33.

EU Gipfel in Brüssel 20.03.2013
Kansela Angela Merkel akihudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa ulaya mjini BrusselsPicha: Reuters

Majina ya watu 12 zaidi ya wale waliotangazwa awali,kwa mujibu wa mwenyekiti wa Umoja wa ulaya Van Rompuy yatatangazwa baadae .

Viongozi wa Umoja wa ulaya wameufutilia mbali mkutano wa kilele uliopangwa kuitishwa June tatu ijao pamoja na Urusi.Hata hivyo wamejizuwia kutangaza vikwazo vya kiuchumi.Viongozi hao wameonya lakini hatua kama hizo zitafuata ikiwa Urusi itazidi kupalilia mgogoro wa Crimea ."Tumaweka wazi kabisa,tuko tayari bila ya shaka kwenda mbali zaidi ikiwa hali itazidi kuwa mbaya -vitakavyofuata wakati huo ni vikwazo vya kiuchumi."Anasema kansela Angela Merkel

Mbali na viongozi wa Umoja wa Ulaya,Marekani pia imezidisha idadi ya warusi na waukrain waliowekewa vikwazo na kufikia 16 na kufungua njia ya vikwazo pia kuwekwa dhidi ya sekta muhimu za uchumi nchini Urusi ikiwa Moscow haitabadilisha mkondo wa mambo kuhusu Ukraine.

Baraza la juu la bunge la Urusi laidhinisha Crimea iwe sehemu ya Urusi

Mjini Moscow kwenyewe lakini baraza la juu la bunge la Urusi limeidhinisha hii leo mpango wa kuijumuisha Crimea na Urusi.Mpango huo ulikwisha idhinishwa kwa wingi mkubwa hapo jana na bunge.Na rais Vladimir Putin amesema nchi yake itajizuwia kwa sasa kutangaza vikwazo kujibu vile vilivyowekwa na Washington.

Putin spricht vor Parlament im Kreml zur Lage in der Ukraine 18.03.2014
Rais Vladimir Putin akihutubia bunge la Urusi Kremlin mjini MoscowPicha: Reuters

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/dpa/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef