1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Ukraine Wazidi Makali

6 Mei 2014

Sauti zinazidi kupazwa kutahadharisha dhidi ya kuripuka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ukraine.Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi,Ukraine na Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kukutana mjini Vienna.

https://p.dw.com/p/1BuQB
Tawi la Benki lahujumiwa na mali kuporwa huko DonetskPicha: DW/K. Oganesian

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza William Hague ,mara baada ya kuwasili mjini Vienna kuhudhuria mkutano wa baraza la Ulaya utakaomulika mgogoro wa Ukraine,ameituhumu Urusi kujaribu kuvuruga uchaguzi wa rais nchini Ukraine.Akizungumza na waandishi habari waziri Hague amesema anataraji "risala kali itatolewa na nyingi kati ya nchi zinazohudhuria mkutano huo, kutaka uchaguzi wa rais uitishwe kama ilivyopangwa."Wananchi wa Ukraine wana haki ya kuwa na serikali yao,rais wao na kuitisha uchaguzi huru na wa kidemokrasia amesema."

Uchaguzi wa rais umepangwa kuitishwa May 25 mwaka huu lakini Moscow imeutaja uchaguzi huo kuwa "hauna maana" huku wanamgambo wananaotaka kujitenga eneo la mashariki wakijiandaa kuitisha kura ya maoni ya kudai uhuru jumapili ijayo.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov hajasema lolote alipowasili Vienna kuhudhuria mkutano huo,wazirio mwenzake lakini wa Ukraine Andriy Deshchytsia amesema:"Tumekuja ili kusaka njia ya kujikwamua toka hali hii iliyoko hivi sasa na kubuni utaratibu utakaotuliza hali ya mambo nchini Ukraine."

Uwezekano wa mafahali wawili kukutana Vienna

Bado si dhahir kama wanasiasa hao wawili waliohudhuria karamu ya chakula cha usiku pamoja na mawaziri wenzao jana usiku mjini Vienna,watakuwa na mkutano baidi pembezoni mwa mkutano huu wa Vienna.

Europarat Wien 2014 6.5.14 Außenminister Treffen Ukraine Andriy Deshchytsia Andre Deshchitsa
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Ukraine Andriy Deshchytsia alipowasili Vienna kuhudhuria mkutano wa baraza la ulayaPicha: Reuters

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Austria alisema mjini Vienna mawaziri Lavrov na Deshtschytsia walikutana kwa muda mfupi,lakini hawakuwa peke yao.

Wakati huo huo Urusi imeongeza idadi ya manuari zake na nyambizi katika eneo la bahari nyeusi,kufuatia kile waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu alichonukuliwa akisema "kumezwa raas ya Crimea.

Vikosi vyaangani na nchi kavu navyo pia vitapelekwa katika vituo vya kijeshi vya Urusi katika bahari nyeusi.

Kitisho cha kuripuka vita vya wenyewe kwa wenyewe

Na nchini Ukraine kwenyewe idadi ya wahanga wa opereshini za kijeshi dhidi ya mji unaodhibitiwa na waasi wa Slavyansk,mashariki ya Ukraine imeongezeka na kufikia watu 34.Kiwanja cha ndege cha Donetsk kimefuingwa-hakuna sababu zilizotolewa.

Außenminister Treffen in Genf 17.04.2014
Mkutano wa mawaziri wa Mambo ya nchi za nje wa Urusi,Ukraine,Marekani na mwakilishi mkuu wa siasa ya nje ya Umoja wa Ulaya uliofanyika Geneva April 17 mwaka huuPicha: picture-alliance/AA

Sauti zinazidi kutolewa kuonya dhidi ya balaa la kuripuka vita vya wenyewe kwa wenyewe.Kuna hofu rais Vladmir Putin asije akaamuru wanajeshi wake waivaamie nchi hiyo jirani.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP/AP

Mhariri:Yusuf Saumu