1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Naibu waziri wa ndani auawa Bolivia

26 Agosti 2016

Naibu waziri wa mambo ya ndani nchini Bolivia, Rodolfo , ameuawa wakati wa maandamano ya wachimba madini , yaliyotokea wakati naibu waziri huyo alipokwenda kusaka suluhu ya mgomo wa wafanyakazi hao wa migodini.

https://p.dw.com/p/1Jq7k
Bolivien Rodolfo Illanes
Rodolfo Illanes- Naibu waziri wa mambo ya ndani Bolivia .Picha: Reuters/Bolivian Presidency

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Bolivia, Carlos Romero, amewaambia waandishi wa habari katika mji mkuu wa taifa hilo la Amerika Kusini, La Paz, kuwa naibu wake aliuawa kinyama. Romero alithibitisha ripoti za walioshuhudia tukio hilo kuwa Illanes, mwenye umri wa miaka 55, alipigwa hadi kufa kufuatia makabiliano kati ya polisi na wachimba migodi hao katika mji wa Panduro ulioko umbali wa kilomita 165 kusini mashariki mwa La Paz.

Romero aliongeza kuwa Illanes ambaye alihudumu katika wadhifa huo wa naibu waziri tangu mwezi Machi, alitekwa nyara na wachimba migodi hao baada ya kujaribu kuanzisha mashauriano nao katika kizuizi cha barabarani. Mlinzi wake pia alijeruhiwa na kupelekwa hospitalini.

Akikitaja kitendo hicho kuwa cha kinyama na ambacho hakijawahi kutokea nchini humo, Waziri wa Mambo ya Ndani Romero pia alitoa wito kwa idara husika ya maswala ya haki kuhakikisha kuwa kifo hicho kinachunguzwa vizuri na kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya wahusika.

Bolivien Protest Minenarbeiter
Jamaa na rafiki waomboleza kifo cha Fermin Mamani, mmoja wa waandamanaji anayedaiwa kufariki baada ya makabiliano na polisi.Picha: picture-alliance/dpa/J. Abrego

Awali Illanes alikuwa amekiambia kituo kimoja cha habari katika eneo hilo kwamba yuko katika hali njema akiwa na watu wake wa karibu na kwamba watu hawawezi kumuumiza. Lakini baadaye ripoti zikasema kuwa ameuawa. Moises Fores, ambaye ni mkurugenzi wa kituo cha redio cha wachimba migodi alisema kuwa waliona maiti ya naibu waziri huyo.

Idadi ya waliofariki na kukamatwa

Mchimba migodi mmoja pia aliuawa katika makabiliano ya hapo jana na kuifanya idadi ya waliofariki kufikia watu wanne tangu kuzuka kwa maandamano hayo kuhusiana na kusajiliwa kwa chama cha wafanyakazi. Wachimba migodi wawili waliuawa siku ya Jumatano.

Takribani wachimba migodi 100 walikamatwa na kuzuiwa baada ya maandamano hayo hapo jana. Kwa sasa wachimba migodi hao wanawakilishwa na vyama huru na ambavyo vimekuwa vikiweka vizuizi vya barabarani huku wakitaka kukubalika kwa haki ya kufanyia kazi kampuni za kibinafsi ama za kigeni.

Katika mahojiano na kituo kimoja cha kibinafsi cha habari, Red Uno, Waziri wa Ulinzi wa Bolivia, Reymi Ferreira, alisema kuwa rais wa nchi hiyo, Evo Morales, alishtushwa sana na habari hizo za kifo hicho, kabla ya kuangua kilio. Aliongeza kuwa aliyeongoza mashambulizi hayo dhidi ya Illanes ametambuliwa na lazima hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika.

Mwanasheria mkuu nchini humo alitangaza kuwa waendeshaji mashtaka watano tayari wametumwa Panduro. Kabla ya mauaji hayo, wachimba migodi hao walikuwa wamekubaliana na serikali kuanza mashauriano kuanzia leo asubuhi katika makao makuu ya makamu wa rais kwa sharti kwamba waondoe vizuizi vyote barabarani.

Mwandishi: Tatu Karema/AFP/dpa
Mhariri: Mohammed Khelef