1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NAIROBI: Kenya yawafukuza Wasomali 18

20 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CP1r

Kenya imewafukuza Wasomali 18 na kuwarudisha mjini Mogadishu. Kwa mujibu wa duru za polisi na kundi moja la kiislamu nchini Kenya, Wasomali wengine 32 wanatarajiwa kurudishwa nchini Somalia.

Wasomali hao waliokimbia mapigano mjini Mogadishu, wamekuwa wakizuiliwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta kwa juma moja baada ya serikali ya Kenya kukataa kuwapa ukimbizi.

Kiongozi wa jukwaa linalopigania haki za waislamu, Al Ami Kimanthi amesema wasomali hao 18 wanalazimishwa kuingia katika ndege itakayowarudisha Mogadishu. Ameishutumu serikali ya Kenya kwa kuvunja sheria za kimataifa kuhusu haki za binadamu kwa kuwafukuza wasomali hao ambao wanatafuta usalama wao.

Kenya iliufunga mpaka wake na Somalia mwezi Januari mwaka huu kuwazuia wanamgambo wa kiislamu waliofukuzwa kutoka Mogadishu na wanajeshi wa serikali ya mpito ya Somali waliosaidiwa na wanajeshi wa Ethiopia.

Jana jioni wanamgambo watatu wa kisomali waliuvamia mji wa Mandera ulio mpakani na kumuua mwanajeshi mmoja wa Kenya na kuwajeruhi wakenya wanne. Wasomali wanne waliuwawa na saba wakajeruhiwa katika ufyatulianaji wa risasi.