1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NAIROBI : Kenyatta hana imani na serikali

7 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CClx

Mtoto wa muasisi wa taifa la Kenya anayetukuzwa marehemu Rais Jomo Kenyatta hapo jana amewasilisha hoja ya kutokuwa na imani na serikali na kuishutumu kwa kupanga njama za kukigawa chama chake pamoja na chama kengine cha kisiasa nchini humo.

Wakati joto la kisiasa likiendelea kupanda kabla ya uchaguzi wa rais mwakani Uhuru Kenyatta amesema serikali ya Rais Mwai Kibaki haina tena mamlaka ya uadilifu na sheria kuongoza nchi.

Akiwasilisha hoja hiyo ya kutokuwa na imani na serikali ambayo matarajio yake yako mashakani kutokana na bunge kuiingia mapumzikoni leo hii Kenyatta amesema serikali inauwa demokrasia ya vyama vingi kwa kupanga mapinduzi ndani ya vyama vya kisiasa.

Kenyatta anadai kwamba serikali ya Kibaki ilishirikiana na Rais wa zamani wa nchi hiyo Daniel arap Moi kumuondowa kwenye wadhifa wa kiongozi wa chama cha KANU na kumpa nafasi hiyo Nicholas Biwott waziri wa zamani alie karibu na Moi anayehusishwa na rushwa.

Mrajisi wa vyama wa serikali wiki iliopita ilimtambuwa Biwott kuwa kiongozi wa KANU jambo ambalo limezusha maandamano ya ghasia mjini Nairobi hapo Jumanne wakati polisi ilipofyatuwa mabomu ya kutowa machozi kutawanya mamia ya wafuasi wa Kenyatta.