1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nairobi. Kibaki azindua kampeni ya kutaka kuchaguliwa tena.

1 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/CBLD

Rais Mwai Kibaki ameahidi kuongeza ukuaji wa uchumi nchini Kenya wakati akizindua kampeni yake ya kutaka kuchaguliwa tena huku maoni ya wapiga kura yakionyesha kuwa yuko katika nafasi ya pili.

Kibaki mwenye umri wa miaka 75 amesema huku akishangiliwa katika mkutano wa chama chake cha PNU katika uwanja wa mpira wa Nyayo mjini Nairobi, kuwa ni muhimu kuwaambia Wakenya ukweli, kuwa nchi hiyo ina hali nzuri zaidi hivi sasa kuliko ilivyokuwa miaka mitano iliyopita , na itakuwa bora zaidi miaka mitano ijayo kutoka sasa chini ya chama cha umoja wa taifa, PNU.

Kibaki , ambaye ni mchumi kitaaluma , amesema serikali yake imefanya bora kwa kiasi kikubwa mazingira ya biashara tangu kuingia madarakani Desemba mwaka 2002 na imefikisha ukuaji wa uchumi katika kiwango cha asilimia 6.1 kwa mwaka.

Lakini mkutano huo , baada ya kutangazwa sana mafanikio yake , umekuja wakati maoni ya wapiga kura nchini humo yakimuweka katika nafasi ya pili nyuma ya mpinzani wake Raila Odinga. Odinga anaongoza chama cha Orange Democratic Movement ODM ambacho kilimpa rais Kibaki kipigo katika kura ya maoni kuhusu katiba mwaka 2005.