1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nairobi. Maafisa wa kupambana na rushwa watakiwa kujiuzulu.

27 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CCyz

Wanaharakati wamedai jana kuwa maafisa wa ngazi ya juu wa kupambana na rushwa nchini Kenya wanapaswa kujiuzulu kuhusiana na hatua za taratibu mno za uchunguzi kuhusiana na kashfa kubwa kabisa ya rushwa katika taifa hilo la Afrika mashariki.

Katika ripoti yao kuhusu rushwa, kundi la mashirika 60 yasiyo ya kiserikali , pamoja na makundi ya kutoa mbinyo wametoa wito wa kujiuzulu kwa mwanasheria mkuu wa serikali Amos Wako na mwenyekiti wa tume ya kupambana na rushwa nchini Kenya Aaron Ringera.

Viongozi hao wawili walipambana mwezi huu juu ya kuwashitaki watu wanaohusika katika kashfa ya Anglo Leasing, ambapo dola milioni 300 zilichukuliwa na kampuni hewa kupitia tenda za serikali.

Kashfa ya Anglo Leasing , ambayo imekuwa mzozo mkubwa tangu pale muungano unaounda serikali ya rais Mwai Kibaki kuingia madarakani mwishoni mwa mwaka 2002 na kulazimisha kujiuzulu kwa mawaziri wawili.