1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NAIROBI: Nchi za Afrika zaonywa kuhusu kutokea tsunami

13 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBQD

Nchi za Afrika katika pwani ya bahari ya Hindi zimeonywa juu ya uwezekano wa kutokea tsunami kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililotokea magharibi mwa pwani ya kisiwa cha Sumatra nchini Indonesia.

Tetemeko hilo la kipimo cha 8.2 katika kipimo cha Richter, limesabaisha vifo vya watu wasiopungua tisa na kuwajeruhi wengine kadhaa kisiwani humo.

Tetemeko lengine la kipimo cha 7.5 limetokea katika kisiwa cha Sumatra, saa 14 baada ya tetemeko la kwanza.

Maafisa nchini Kenya wamewashauri raia wanaoishi katika mwambao wa pwani wasikaribie maeneo ya baharini na wawe katika hali ya tahadhari.

Msemaji wa serikali, Alfred Mutua, ambaye awali alisema tsunami inatarajiwa kupiga pwani ya Kenya mwendo wa saa tano na dakika 39 usiku wa kuamkia leo, amepunguza kitisho cha kutokea tsunami hiyo.

Tanzania pia imetoa onyo ikiwataka wananchi wanaoishi katika mwambao wa pwani na visiwa vya Zanzibar na Pemba wajihadhari.

Mauritius imetoa onyo la tsunami ikiwataka raia wasiende kwenye maeneo ya pwani.