1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nairobi. Odinga mgombea wa ODM katika uchaguzi.

2 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBTZ

Chama kikuu cha upinzani nchini Kenya cha Orange Democratic Movement ODM, jana kimefanya uteuzi wa mgombea wake katika kiti cha urais kwa kumchagua mwanasiasa mwandamizi Raila Odinga kuwa mgombea wake wa kiti hicho, wakati kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka huu zikipata kasi.

Kiasi cha wajumbe 4200 wa chama cha ODM walimchagua Odinga , mwenye umri wa miaka 62 , akiwa mtoto wa makamu wa kwanza wa rais nchini humo, ambaye anafanya juhudi zake za mara ya pili kuwania kiti hicho.Odinga ambaye amewaangusha wagombea wengine watatu, alimtaja waziri wa zamani wa fedha na ambaye aliwahi kuwa makamu wa rais Musalia Mudavadi kuwa naibu wake.

Katika hotuba yake ya kukubali uteuzi huo , Odinga aliishutumu serikali ya rais Mwai Kibaki kwa kile alichosema kuwa ni kushindwa kutatua matatizo yanayolikabili taifa hilo la Afrika mashariki, lenye wakaazi milioni 34.

Wakati huo huo mtoto wa rais wa zamani nchini Kenya Daniel arap Moi ametishia kulishtaki gazeti la Uingereza ambalo lilidai kuwa baba yake na washirika wake waliiba kiasi cha dola bilioni moja wakati wa utawala wake.

Gideon Moi amesema kuwa atalishtaki gazeti la Guardian ambalo lilisema kuwa familia ya Moi, makampuni ya Shell, wakfu za siri, watu wa karibu na rais pamoja na washirika walijipatia kiasi cha dola bilioni moja na kuzipeleka nje ya nchi katika utawala wa miaka 24 wa rais Moi ambao ulimalizika mwaka 2002.