1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NAIROBI : Ufaransa kulinda meli za chakula kwa Somalia

27 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBMG

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa WFP limekaribisha pendekezo la Ufaransa kusaidia kuzilinda meli dhidi maharamia wakati zikisafirisha msaada wa chakula unaohitajika mno kwa Somalia.

Mkurugenzi mtendaji wa WFP Josette Sheeran amesema katika taarifa leo hii kwamba wanaishukuru serikali ya Ufaransa kwa ukarimu huo ambao utapunguza tishio la uharamia kuliruhusu shirika hilo la WFP kuweza kulisha watu zaidi wanaokabiliwa na njaa nchini Somalia.

Chini ya pendekezo hilo la Ufaransa WFP imesema manowari za Ufaransa zitasindikiza meli zenye kubeba chakula cha shirika hilo katika bahari ya Somalia kwa miezi miwili na kuandamana nazo hadi bandari ya Mogadishu ambayo inalindwa na wanajeshi wa Uganda kutoka kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika.

Njia ya bahari ya mwambao wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika ni ya hatari kabisa duniani na inaonyesha kutokuwepo kwa utulivu ndani ya nchi hiyo ambapo serikali dhaifu ya mpito inajitahidi kuweka mamlaka yake wakati ikipambana na waasi wa Kiislam.