1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NAIROBI:Manusura wa Gatumba kuanza maisha Marekani

19 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCHY

Kundi la kwanza la manusura 35 kufuatia mauaji ya Gatumba nchini Burundi wanaanza maisha mapya nchini Marekani katika mpango wa Shirika la Umoja wa mataifa la wakimbizi UNHCR.Takriban wakimbizi 160 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo walichinjwa kinyama na kuteketezwa hadi kufa na waasi wa KiHutu walioshambulia kambi moja iliyokuwa kwenye eneo la mpakani mwezi Agosti mwaka 2004.

Wengi wa waliouawa walikuwa wanawake na watoto.Manusura 500 wanapewa nafasi ya kuanza maisha upya nchini Marekani katika mpango unaoshirikisha serikali ya nchi hiyo na Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa mwakilishi wa Shirika la wakimbizi la Umoja wa mataifa UNHCR Kaba-Guichard Neyaga mpango huo utahakikisha kuwa watu hao wanapata huduma za matibabu vilevile kuhakikishiwa usalama wao.

Watu hao walipata mafunzo ya lugha ya Kiingereza kabla kuelekea miji ya Denver na San Francisco ambako mashirika ya misaada yatawasaidia kuanza maisha upya vilevile ujuzi wa kupatia kazi.Kwa mujibu wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa ,UNHCR yapata watu 100 watasafiri kila wiki kuelekea Marekani mpaka mpango huo kukamilika ifikapo mwezi Aprili.