1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Namna Kenya ilivyopokea taarifa ya Ocampo.

16 Desemba 2010

Watu hao sita ni Mawaziri wawili, Waziri wa zamani, Mkuu wa zamani wa Polisi, Mkuu wa utumishi wa umma na mwanahabari.

https://p.dw.com/p/QcmL
Luis Moreno Ocampo, alitaja watu sita kama washukiwa wakuu wa ghasia za uchaguzi Kenya.Picha: dpa - Fotoreport

Muda mfupi tu baada ya Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya kimataifa ya Uhalifu ICC Luis Moreno Ocampo kuwataja watu sita wanaoshukiwa kuwa wahusika wakuu katika ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 nchini Kenya, viongozi wametoa hisia zao. Rais Mwai Kibaki alisema watu hao sita waliotajwa, ikiwemo mawaziri wawili na Mkuu wa Utumishi wa Umma, bado hawajafanyiwa uchunguzi wa kutosha kwa sababu shughuli hiyo ya kuwashtaki haijaanza rasmi huko The Hague. Rais Kibaki aliongeza kuwa mwito uliotolewa na Ocampo kutaka washukiwa hao sita kuchukuliwa hatua una madhara na unakwenda kinyume na haki zao za kimsingi. Meja Generali Hussein Ali, ambaye alikuwa Mkuu wa Polisi amesema alifanya majukumu yake ipasavyo na kwamba  mashtaka dhidi yake hayana msingi. Wengine pia waliotupilia mbali tuhuma dhidi yao ni Uhuru Kenyatta ambaye ni Waziri wa Fedha, William Ruto Waziri wa zamani wa elimu ya juu na Francis Muthaura Katibu wa baraza la Mawaziri na mkuu wa utumishi wa umma nchini Kenya.