1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Namna ya kumlinda mtoto na Ukimwi

19 Agosti 2014

Wataalamu wa afya barani Afrika wanawashauri kina mama wenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutumia uzazi wa mpango ili kuhakikisha wanamlinda mtoto na maambukizi ya vurusi vya ukimwi.

https://p.dw.com/p/1Cx6h
Symbolbild Schwangerschaft Leihmutter
Wanawake wenye uja uzitoPicha: NICOLAS ASFOURI/AFP/Getty Images

Hatua hiyo ikiaminika kuwa uzazi wa mpango ni nguzo ya pili ya mafanikio ya kuzuia maambukizi ya mama kwa mtoto.

Kwa mujibu wa Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa, UNFPA, uzazi wa mpango ni muhimu katika mataifa ya kusini na mashariki mwa Afrika, ambako maambukizi ya Virusi vya Ukimwi,VVU, ni makubwa.

Umuhimu wa kuwatunza watoto walioambukizwa

Florence Ngobeni Allen ni msemaji wa taasisi ya Elizabeth Glaser Paediatric AIDS Foundation ameliambia shirika la habari la IPS kuwa pamoja na kuzuia maambukizi miongoni mwa wanawake na watoto na kuwatunza wale walioambukizwa, uzazi wa mpango kwa wanawake wenye VVU una lengo la kuwaweka mama na mtoto kwenye afya. Ngobeni anatolea mfano wa Afrika Kusini ambako mnamo mwaka 1996 mama mmoja mwenye maambukizi ya VVU alipoteza mtoto, lakini sasa ana watoto wawili wa kiume wakubwa na wenye afya.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyopewa jina la "Women Out Loud" inasema tafiti zinaonyesha kuwa wanawake wanaoishi na VVU wana hisia sawa na wale wasio na maambukizi hayo, ikiwemo haja ya kupata watoto, lakini wanahofia usalama wao na wa mtoto. Robo tatu ya wanawake wanaoishi na VVU katika nchi za Kenya na Malawi hawakutaka watoto zaidi ndani ya miaka miwili ijayo, lakini robo yao hutumia njia za kisasa za uzazi.

Waathiriki hawana mpango wa uzazi

Utafiti uliofanywa na shirika la Family Health International ulibaini kuwa zaidi ya nusu ya wanawake wenye VVU nchini Rwanda na Afrika Kusini, hawakuwa na mpango wa ujauzito hivi karibuni.

Südafrika Mutterschaft Teenager
Mama akiwa na mtoto mchangaPicha: AP

Licha ya kuwa wanawake hao walitaka uzazi wa mpango, lakini upatikanaji wake ulikuwa mgumu na miongoni mwa vizuizi ni wafanyakazi wa afya, ambao walishindwa kutoa mafunzo ya uchaguzi wa njia za uzazi wa mpango kwa wanawake wanaoishi na maambukizi ya VVU.

Pili ni imani potofu juu ya usalama wa uzazi wa mpango kwa wanawake wanaoishi na VVU kwa kutolewa zaidi mipira ya kinga ya kiume pekee, licha ya kuwa wanawake walipendelea njia za uzazi wa mpango za muda mrefu ikiwemo ya sindano na vipandikizi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Msaidizi wa Hospitali ya Taifa ya Kenyatta nchini Kenya, Dk John Ong'ech, asilimia 25 kati ya wanawake asilimia 60 wanaoishi na virusi vya Ukimwi hawajafikiwa na elimu ya uzazi wa mpango.

Wataalamu wanashauri kuwepo kwa kile kinachoitwa vituo vya "One Stop" ambavyo vinaunganisha huduma za ushauri juu ya VVU, uzazi wa mpango na huduma za uzazi pamoja na afya ya mtoto ili kuokoa muda kwa wahitaji huduma na watumishi wa afya.

Nchi saba za kusini mwa Afrika zimejiandaa kuanzisha vituo hivyo kwa ajili ya afya ya uzazi, na hivyo kuwa na eneo ambapo mhudumu mmoja wa afya anaweza kumparia mama mwenye VVU dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo, kumfanyia uchunguzi wa kansa ya shingo ya kizazi, na pia kumpa ushauri kuhusu uzazi wa mpango.

Na kwa mujibu wa Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa, UNFPA, kuunganisha huduma hii ni gharama nafuu na yenye ufanisi zaidi.


Mwandishi: Zuhura Hussein/IPS
Mhariri: Mohammed Khelef