1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nancy amupelekea Assad wa Syria ujumbe kutoka Israel

Maja Dreyer4 Aprili 2007

Akiwa ziarani yake nchini Syria, spika wa bunge la Marekani, Bibi Nancy Pelosi, aliwasilisha mualiko wa serikali ya Israel wa kuwa na mazungumzo ya amani na Syria. Kwa mujibu wa Bi Pelosi, rais wa Syria Bashar el Assad amekubali mazungumzo hayo. Ziara ya Pelosi nchini Syria imekosolewa vikali na rais Bush wa Marekani.

https://p.dw.com/p/CHGv
Nancy Pelosi na Bashar al Assad
Nancy Pelosi na Bashar al AssadPicha: AP

Ujumbe wa Israel ambao spika wa bunge la Marekani, Bi Nancy Pelosi, alimpelekea rais Assad wa Syria unasema Israel iko tayari kwa mazungumzo ya amani. Haya aliyasema Bibi Pelosi baada ya mkutano wake na rais Assad mjini Damaskus.

Katika mkutano huo huo, Assad alimhakikishia Pelosi kwamba yeye pia anakaribisha mazungumzo haya na Israel.

Bi Pelosi alikutana na rais Assad kwenye ikulu yake milimani karibu na Damaskus. Baada ya hapo, Pelosi alisema yalikuwa mazungumzo mazuri yaliyohusu hasa juhudi za kuleta amani Mashariki ya Kati. Kama alivyoarifu awali, Bi Pelosi pia alitaja wasiwasi wake juu uungaji mkono wa Syria kwa makundi ya Kiislamu ya msimamo mkali ya Hamas na Hizbollah.

Kwa kuitembelea Syria Bi Pelosi ambaye pia ni kiongozi wa upinzani nchini Marekani hakujali ukosoaji wa rais wa Marekani George W. Bush. Bush alimshutumu Bibi Pelosi kwa kuziathiri sera za nchi za nje za Marekani. Kwa kuitembelea Syria anadhoofisha juhudi za serikali yake kuitenga serikali ya Syria. Baada ya kuuawa waziri mkuu wa Lebanon Rafik Hariri mnamo mwaka 2005 Marekani iliisusia Syria. Wachunguzi wa Marekani wanaona kuwa idara ya ujasusi ya Syria inahusika katika mauaji haya. Syria lakini imeyakanusha hayo.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, rais Bush alisisitiza kuwa Syria haiwazuii wanamgambo kuingia katika Iraq wakitokea Syria na pia inavuruga amani nchini Lebanon.

Bibi Pelosi ambaye anachukua nafasi ya tatu katika safu za madaraka nchini Marekani alisema mkutano wake na rais Assad ni muhimu katika kuanzisha upya mazungumzo juu ya Iraq na Lebanon.

Nancy Pelosi alisema: “Jukumu la Syria nchini Iraq, jukumu la Syria katika kuyaunga mkono makundi ya Hamas na Hizbollah, jukumu la Syria kwa kweli ni kubwa, kwa hivyo tunaamini kuna uwezekano mkubwa wa kuiboresha hali ya mambo.”

Wajumbe wa serikali ya Syria walisema wanataka kuisaidia Marekani kuondoka Iraq kwa heshima. Kama malipo inaitaka Merakani kuishinikiza Israel itoke kutoka milima ya Golan ambayo Israeli inaikalia miaka 40 iliyopita. Alipozungumza na waandishi wa habari, waziri wa nchi za nje wa Syria, Walid al-Moualem alisema na hapa ninamnukuu: Walisema Bw. Olmert yuko tayari kwa amani na Syria. Sisi tulijibu Syria iko tayari kwa amani kulingana na masharti yaliyowekwa na umoja wa nchi za Kiarabu.” - mwisho wa kumnukuu waziri al-Moualem.

Mazungumzo ya amani kati ya Israeli na Syria juu ya suala la milima ya Golam yalisitishwa mwaka 2000. Afisa wa serikali ya Israeli aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa Pelosi kwenye ziara yake nchini Israeli aliyoifanya kabla ya kwenda Syria, alimuuliza waziri mkuu Olmert ikiwa ana ujumbe wowote wa kuupeleka Syria. Katika matamshi yake ya mwisho kuhusiana na suala la amani na Syria, mwezi wa Disemba Bw. Olmert alisema amani inategemea Syria kusitisha uhusiano wake na Iran pamoja na uungaji mkono kwa Hamas na Hizbollah. Rais Assad wa Syria amesisitiza mara kwa mara kuwa amani katika Masharika ya Kati haitakuwepo bila ya Syria kuhusishwa.