1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani atakaelipa gharama za maafa ya Ghuba ya Mexico?

19 Julai 2010

Kama kampuni kubwa kabisa ya mafuta BP isingepata faida kubwa miaka hii iliyopita, basi ingefilisika kwa sababu ya maafa makubwa ya mafuta yaliyotokea katika Ghuba ya Mexico nchini Marekani.

https://p.dw.com/p/OPR6
In this image made from video provided by British Petroleum (BP PLC), Wednesday, June 2, 2010, shows the site of the Deepwater Horizon oil spill. (AP Photo/BP PLC)
Mafuta yaliyokuwa yakitiririka baharini kutoka kisima cha mafuta katika Ghuba ya Mexico.Picha: AP

Hata hivyo, moja ni dhahiri: janga hilo litaigharimu BP fedha nyingi sana, kwani ni matumaini ya wakaazi wa maeneo yaliyoathirika kuwa ahadi zilizotolewa na kampuni hiyo ya Uingerza,katika mwezi wa Mei,zitaheshimiwa. Kampuni ya BP itakabiliwa na gharama kubwa kweli, kwani kwa mujibu wa sheria mojawapo ya Marekani, kampuni hiyo ya Kingereza inaweza kuwajibishwa kulipa hadi dola 27 kwa kila lita ya mafuta yaliyotiririika baharini katika Ghuba ya Mexico, kufuatia ajali iliyotokea mwezi wa Aprili. Kwa hivyo, wakosoaji wa BP wana wasiwasi kuwa kampuni hiyo inataka kuficha ukweli kuhusu kiwango cha mafuta yaliyovuja kutoka kisima hicho.

Kwa mujibu wa BP, kampuni hiyo tayari imeshalipa takriban dola bilioni tatu na nusu kusaidia kusafisha maeneo yaliyochafuka kwa mafuta, kuzuia mafuta kutiririka zaidi baharini pamoja na kuwalipa fidia wakaazi wa maeneo ya pwani katika Ghuba ya Mexico. Kampuni hiyo imeshakubaliana na serikali ya Marekani kuanzisha mfuko maalum wa msaada, kwa kutoa dola bilioni 20. Sehemu ya fedha hizo zitatumiwa kuwalipa wavuvi waliopoteza ajira kwa sababu ya maafa yaliyochafua mazingira. Watalipwa kwa miaka minne ijayo, lakini haijulikani kama fedha hizo zitatosha. Kwa hivyo, Rais wa Marekani Barack Obama ametamka waziwazi kuwa kitita hicho cha dola bilioni 20, hakimaanishi kuwa kampuni ya BP haitowajibika tena kwa mengine. Akaongezea:

President Barack Obama makes a statement on the capping of the BP well in the Gulf, Friday, July 16, 2010, in the Rose Garden at the White House in Washington, (AP Photo/Susan Walsh)
Rais Barack Obama akitoa taarifa kuhusu jitahada za BP kuziba kisima cha mafuta katika Ghuba ya Mexico.Picha: AP

"BP italipa hasara zilizosababishwa na kampuni hiyo. Si kwa hasara ya mazingira tu bali hata gharama za kusafisha maeneo yaliyoathirika. Vile vile lazima itoe fidia kwa wakaazi wanaoteseka kwa sababu ya ajali hiyo ya mafuta."

Wakaazi wa maeneo ya pwani yaliyoathirika, wana wasi wasi kuhusu mustakabali wao. Wengi wao na hata maafisa wa kanda hiyo ya pwani hawakuridhika na maafikiano yaliyopatikana kati ya serikali ya Marekani na kampuni ya BP. Kwa hivyo, serikali ya jimbo la Louisiana imeshaandika barua mbili kuiomba kampuni hiyo, dola milioni 10 kuwahudumia kimatibabu wavuvi waliopoteza ajira na kuathirika kiakili. Lakini hadi sasa, hakuna hata senti moja iliyotolewa. Wavuvi wala hawajui lini wataweza kwenda kuvua tena. Mafuta yaliyomiminika baharini yamehatarisha mfumo wa ekolojia na hifadhi kumi na mbili za wanyama. Hoteli na mikahawa ipo tupu, kwani watalii wanalikimbia eneo hilo. Ni dhahiri kuwa itachukua miaka mingi mno, kwa sekta hizo kujirekebisha.

Mwandishi: Hammer,Benjamin

Mhariri: Charo,Josephat