1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

National Front chaangushwa Ufaransa

14 Desemba 2015

Chama cha siasa za mrengo wa kulia nchini Ufaransa, National Front - FN, kimeshindwa katika duru ya pili ya uchaguzi wa majimbo nchini humo, bila kupata hata jimbo moja

https://p.dw.com/p/1HMqi
Frankreich Zweite Runde der Regionalwahlen 2015 Marine Le Pen
Picha: Reuters/Y. Herman

Hayo ni licha ya kutawala katika duru ya kwanza mwishoni mwa wiki iliyopita. Huku uchaguzi wa rais ukitarajiwa mwaka wa 2017, chama cha FN kinachopinga uhamiaji kilitarajia kuwa uchaguzi huu wa majimbo ungetumika kama mwanzo wa safari ya kiongozi wake Marine Le Pen.

Licha ya FN kuwa na matokeo mazuri katika kura za kitaifa, Le Pen aliangushwa na upinzani wa mrengo wa kulia katika jimbo la Nord-Pas-de-Calais-Picardie baada ya chama tawala cha Kisioshaliti kujiondoa katika kinyang'anyiro kabla ya duru ya pili. Le Pen alielezea matumaini licha ya kushindwa. Le Pen amesema "Matokeo ya mwanzo thabiti yalipatikana tangu raundi ya kwanza na kusababisha kutokomezwa moja kwa moja toka ngome zao za kaskazini na kusini mashariki chama cha Kisoshialisti cha eneo hilo, ambacho hakikuwa na faida kwa yeyote".

Le Pen amesema ikilinganishwa na uchaguzi wa mwisho wa majimbo mwaka wa 2010, orodha zao zimepata kura zaidi kutoka asilimia 9.17 hadi asilimia 30 katika duru ya pili, ikiwa ni baada ya miaka mitano pekee. Mpwawe aliye na umri wa miaka 26 Marion Marechal-Le Pen pia alishindwa katika jimbo la kusini ambalo lina pia maeneo ya kifahari kama vile Cote d'Azur, licha ya kutawala katika duru ya kwanza wiki iliyopita

Frankreich Zweite Runde der Regionalwahlen 2015 Marine Le Pen
Picha: Reuters/Y. Herman

Chama hicho kilishinda kura katika majimbo sita kati ya 13 mnamo Desemba 6, kikiwa na asilimia 28 ya mgao wa kura kitaifa, iliyochochewa na ghadhabu kuhusiana na uchumi unaoyumba na wasiwasi uliozuka kufuatia mashambulizi ya kigaidi ya mwezi uliopita mjini Paris yaliyowauwa watu 130.

Lakini mwezi mmoja baada ya mashambulizi hayo, wapiga kura walijitokeza kwa wingi – karibu asilimia 58 walishiriki, ikiwa ni juu kutoka asilimia 50 iliyojitokeza katika duru ya kwanza – na kwa mara nyingine wakakiangusha FN katika mkondo wa mwisho. Waziri Mkuu Msoshialisti Manuel Valls ameonya kuwa licha ya matokeo hayo "kitisho cha chama cha siasa za mrengo wa kulia cha FN bado hakijaondolewa kabisa".

Sarkozy, kiongozi wa chama cha Republican amewapongeza wapiga kura lakini naye akasema kuwa onyo lililojitokeza katika duru ya kwanza halipaswi kusahaulika. "Sasa tunapaswa kuchukua muda kwa ajili ya majadiliano ya kina kuhusu kinachowapa wasiwasi Wafaransa – ambao wanatarajia majibu imara na ya kweli – na ambayo tunawajibikia. Ninatafakari kuhusu Ulaya, sera ya uchumi, ukosefu mkubwa wa ajira, usalama wetu, namna elimu ya watoto inavyoendeshwa, na utambulisho wetu".

Chama tawala cha Kisoshialisti cha Rais Francois Hollande kilishinda katika majimbo matano, huku muungano wa siasa za wastani za mrengo wa kulia wa mtangulizi wake Nicolas Sarkozy kikinyakua majimbo saba. Chama cha Wazalendo kilishinda jimbo la Corsica.

Mojawapo ya matokeo ya kushangaza katika uchaguzi huo ni katika jimbo la Paris, ambao ulihama kutoka mrengo wa kushoto na kwenda wa kulia kwa mara ya kwanza katika miaka 17.

Matokeo ya mwisho yalionyesha kuwa Le Pen alishinda karibu asilimia 42 dhidi ya karibu asilimia 58 ya mpinzani wake wa mrengo wa kulia Xavier Bertrand katika upande wa kaskazini wenye matatizo ya kichumi.

Katika hotuba yenye jazba baada ya vituo vya kura kufungwa, Le Pen alisema hakuna kitakachowazuia sasa.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Gakuba Daniel