1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yaendeleza mashambulizi Libya

25 Mei 2011

Jumuiya ya kujihami ya NATO imeendelea kufanya mashambulio, makali katika maeneo ya mji mkuu wa Libya kwa zaidi ya miezi miwili sasa, huku shinikizo la kumuondoa madarakani Gaddafi likiongezeka.

https://p.dw.com/p/11Njq
Moshi umetanda katika anga ya mji wa Tripoli, baada ya mashambulizi ya NATO
Moshi umetanda katika anga ya mji wa Tripoli, baada ya mashambulizi ya NATOPicha: picture alliance/dpa

Shinikizo kutoka kwa Ufaransa na Marekani za kutaka kuufikisha kikomo utawala wa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi zimeshika kasi.

Jana jioni milio mikubwa ya miripuko takribani 6 ilisikika kwa kiasi cha dakika kumi baada ya mashambulizi ya nguvu yaliofanywa kwa kipindi cha masaa 24 yaliyopita, ambayo yaliathiri makazi ya Gaddafi na ambapo maafisa wa Libya walisema watu 19 wameuwawa.

Shirika la Habari la Libya, JANA, limesema mashambulio hiyo pia yamefanyika katika msikiti mmoja mjini Tripoli unaoitwa Nuri Bani, taarifa ambayo haikuweza kuthibitishwa na vyombo huru vya habari.

EU Außenministertreffen in Luxemburg Alain Juppe
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Alain JuppePicha: dapd

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Alain Juppe, amesema Mashambulio ya Umoja wa Kujihami wa NATO yanaonesha maendeleo, na yanaweza kufikia malengo yake katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja.

Ufaransa, Uingereza na Marekani wanaongoza mashambulizi hayo ya anga ambayo yalianza Machi 19 baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa ridhaa ya " kuchukuliwa hatua zote muhimu" kuwalinda raia dhidi ya majeshi ya Gaddafi, ambae amekuwa akiwakandamiza wanamageuzi wanaoupinga utawala wake wa miaka 41.

Nchi hizo tatu zimeapa kuendelea na kampeni yao dhidi ya Gaddafi mpaka aondoke madarakani.

Aidha kwa upande wao, Marekani inaimarisha hadhi ya Baraza la Mpito la Waasi kama serikali inayotarajiwa baada ya kuliruhusu kufungua ofisi zake mjini Washington.

Jitihada za kidiplomasia pia zinaendelea katika namna tofauti. Nchi za G8 ambazo ni mataifa yenye nguvu duniani wanatarajiwa kujadili hatima ya Libya katika mkutano wake wikii hii, ambapo Urusi inategemewa kuwasilisha mapendekezo ya upatanishi.

Vyanzo vingine vya habari vinasema Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini wiki ijayo anatarajiwa kwenda mjini Tripoli kwa lengo la kupanga mikakati ya namna ya kuondoka kwa Gaddafi nchini humo.

Na wakuu wa mataifa ya Afrika leo wanakutana huko Addis Ababa, nchini Ethiopia.

Jacob Zuma Brüssel Belgien Südafrika Gipfel
Rais wa Afrika ya Kusini Jacob Zuma,Picha: picture-alliance/dpa

Mapema April, rais Zuma alifanya jaribio la kusitisha mapigano nchini Libya, jambo lililopingwa vikali na waasi, wakisema hawana imani na Gaddafi kuendelea kuwepo nchini humo.

Wakati huo huo, wakosoaji wanasema NATO imevuka mipaka ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Matiafa katika operesheni zake nchini Libya, huku waasi wakilalamika kuwa opereshi ya nchi za magharibi haijatekelezwa kwa kiasi cha kutosha katika kulivunja nguvu kabisa jeshi la Gaddafi.

Pamoja na hayo yote, Gaddafi mwenyewe amesikika mara kadhaa akikanusha kwamba wanajeshi wake wanashambulia raia wasio na hatia na kusema waasi ambao wanayadhibiti maeneo ya mashariki ambayo yana utajiri wa mafuta kuwa ni wahalifu, wana itikadi kali za kidini na ni wanachama wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda.

Mwandishi: Sudi Mnette/Reuters
Mhariri: Miraji Othman