1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yashtushwa na Urusi kuhusu Syria

Mohammed Khelef10 Septemba 2015

Gazeti moja mashuhuri nchini Urusi limethibitisha nchi hiyo kuusaidia kijeshi utawala wa Rais Bashar al-Assad, huku Jumuiya ya Kujihami ya NATO ikihofia kuimarika kwa dhima ya Urusi nchini Syria.

https://p.dw.com/p/1GU6K
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg.Picha: DW

Ripoti za gazeti hilo la Kommeesan linaloheshimika nchini Urusi, ambalo linasema vyanzo vyake ni watu waliomo kwenye shirika la usafirishaji silaha la la nchi hiyo, inakuja wakati serikali ya Rais Vladimir Putin ikisema msaada wake wa kijeshi kwa serikali ya Syria unadhamiria tu kupambana na ugaidi.

Shirika la usafirishaji silaha la Urusi halikupatikana mara moja kuzungumzia shutuma hizi mpya, lakini mataifa ya Magharibi yanasema utawala wa Rais Putin unajaribu kujenga himaya yake nchini Syria hivi sasa ili kumlinda Rais Assad.

Miongoni mwa silaaha ambazo zimo kwenye shehena zilizofikishwa Syria hadi sasa ni bunduki ndogo ndogo, mizinga ya kurushia mabomu, magari ya kijeshi ya kiwango cha juu chapa BTR-82A na malori aina ya Kamaz.

NATO yaja juu

Vyanzo kwenye ripoti hiyo vinasema serikali ya Syria ilikuwa tayari imeshalipia manunuzi ya mifumo ya ulinzi wa anga aina ya S-300, lakini baadaye Urusi iliamua kutokuwasilisha mifumo hiyo ya kurusha makombora na badala yake ikatuma silaha nyenginezo.

Rais Vladimir Putin wa Urusi.
Rais Vladimir Putin wa Urusi.Picha: picture-alliance/dpa/M. Metzel

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg, amesema shirika lake lina taarifa za harakati hizo za kijeshi za Urusi nchini Syria.

"Nina wasiwasi sana na kuongezeka kwa shughuli za kijeshi za Urusi nchini Syria. Jambo hili halitachangia utatuzi wa mgogoro uliopo. Nadhani sasa ni muhimu kuunga mkono jitihada zote za kusaka suluhisho la kisiasa kwa mzozo huu, nasi tunaunga mkono sana juhudi za Umoja wa Mataifa kutafuta suluhisho hilo la kisiasa," alisema Katibu Mkuu huyo wa NATO, ingawa alikataa kuzungumzia suala la mifumo ya ulinzi wa anga akisema linahusiana na dhamana ya taifa husika, ingawa Syria ni jirani wa Uturuki, mwanachama wa NATO anayeweza kuathirika moja kwa moja na mifumo hiyo lau ingetumika.

Kutoka nchini Lebanon, jirani mwengine wa Syria, vyanzo vya habari vinasema wanajeshi wa Urusi wenyewe ndio wanaoshiriki kwenye operesheni za kijeshi ndani ya Syria hivi sasa kuvisaidia vikosi vya serikali. Hilo linathibitisha taarifa za kijasusi za Marekani kwamba Urusi inamsaidia kijeshi Rais Assad.

Marekani yenyewe inapigana dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu nchini Syria hivi sasa huku pia ikipingana na utawala wa Assad.

Mbali na kuzalisha mamilioni ya wakimbizi, vita vya miaka minne nchini Syria vimeshaangamiza maisha ya zaidi ya watu 250,000 kwa mujibu wa hisabu za Umoja wa Mataifa, vikiwa havina dalili yoyote ya kumalizika kwa karibu na huku vikizidi kuchochewa na mikono kutoka nje.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf