1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yautwanga tena mji wa Tripoli

24 Mei 2011

Usiku wa kuamkia leo (24 Mei 2011) ndege za Jumuiya ya Kujihami ya NATO zilifanya mashambulizi makubwa katika mji mkuu wa Tripoli, ambayo yanatajwa kuwa mabaya zaidi tangu NATO ianze operesheni yake dhidi ya Gaddafi.

https://p.dw.com/p/11MYy
Moto na moshi kwa mashambulizi ya NATo mjini Tripoli
Moto na moshi kwa mashambulizi ya NATo mjini TripoliPicha: dapd

Kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Libya, Moussa Ibrahim, watu watatu wameuawa kutokana na mashambulizi hayo na wengine 150 wamejeruhiwa, wengi wao wakiwa raia. Moussa ameuita usiku wa jana kuwa ni "usiku mwengine wa mauaji ya NATO."

Mashahidi wanasema kwamba ndege za NATO zilirusha makombora yapatayo 20 kwa kipindi cha nusu saa mfululizo, huku shabaha zikielekezwa maegesho ya ndege za kijeshi za vikosi vya Kanali Gaddafi, mjini Tripoli. Mashahidi hao wameongeza kuwa ndege za NATO ziliruka umbali mdogo tu juu ya anga ya Libya.

Mapema Ufaransa iliamua kupeleka helikopta za kijeshi, ambazo msemaji wa wizara ya ulinzi ya Ufaransa, alisema kwamba ni rahisi kulenga maghala ya silaha au vifaru vya Gaddafi vilivyojichanganya kwenye maeneo yenye raia kwa ufanisi.

Kwa mujibu wa msemaji huyo, hili litasaidia kupunguza maafa kwa raia wa kawaida, ambao hadi sasa wamekuwa wakitajwa kujikuta wahanga wa mashambulizi hayo ya NATO yaliyokusudiwa kuwalinda.

Kwa mujibu wa magazeti nchini Ufaransa, helikopta 12 za jeshi la nchi hiyo ziko kwenye meli hivi sasa zikielekea pwani ya Libya.

Meli ya kivita ya Libya baada ya kushambuliwa na maroketi ya NATO hivi karibuni
Meli ya kivita ya Libya baada ya kushambuliwa na maroketi ya NATO hivi karibuniPicha: AP

Tangu mwishoni mwa mwezi Machi, ndege za NATO zimekuwa zikishambulia karibuni mfululizo maeneo kadhaa wanayosema kwamba ni ama maghala ya silaha au vituo vya kuendeshea vita vya Kanali Gaddafi, katika operesheni ya kuwalinda raia wa Libya dhidi ya vikosi vya serikali.

Hatua ya sasa ya Ufaransa kupeleka helikopta za kijeshi inachukuliwa kuwa karibu sana na kuingiza vikosi vya miguu nchini Libya, ingawa NATO imekuwa ikishikilia kuwa haina dhamira hiyo.

Rais wa Marekani, Barack Obama na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, wameendelea kusisitiza kwamba ni lazima Gaddafi aondoke madarakani, huku wakisema kwamba operesheni ya kijeshi dhidi ya kiongozi huyo itaendelea hadi hapo dunia itakaporidhika kwamba azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetekelezwa kikamilifu.

Katika hatua nyengine, waasi wa Libya wamekubali mualiko wa Marekani kufungua ofisi yao jijini Washington. Kwa mujibu wa Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje, Jeffrey Feltman, yeye mwenyewe ndiye aliyewakabidhi ombi hilo waasi, ambalo waasi hao wamelipokea.

Feltman yuko kwenye ziara ya siku tatu mjini Benghazi kwa mazungumzo na viongozi wa waasi hao.

Mwandishi: Thomas Bohrmann/ZPR/AFP
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman