1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nawaz Sharif awasili Jeddah Saudi Arabia

10 Septemba 2007

Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Nawaz Sharif amewasili nchini Saudi Arabia katika mji wa Jeddah baada ya kufukuzwa nchini Pakistan.

https://p.dw.com/p/CB1Q
Akilakiwa na wafuasi wake alipofika Islamabad kabla ya kurudishwa Saudia
Akilakiwa na wafuasi wake alipofika Islamabad kabla ya kurudishwa SaudiaPicha: AP

Sharif alirudishwa nchini Saudi Arabia saa chache baada ya kuingia Pakistan kutoka Uhamishoni akiwa na lengo la kutaka kufanya kampeini ya kumuondoa madarakani rais Musharaf.

Nawaz Sharif alirudishwa Saudi Arabia leo hii saa chache baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Islamabad.

Lengo kuu la kiongozi huyo wa zamani wa Pakistan lilikuwa moja tu kuanzisha kampeini kabambe ya kumuondoa madarakani rais Pervez Musharraf.

Katika tukio la aina yake Sharif mwenye umri wa miaka 57 alikataa katakata kutoa pasi yake ya kusafiri kwa maafisa wa usalama jambo ambalo lilizusha mvutano kati yake na maafisa wa polisi ambao walimkamata na kumpandisha kwenye ndege ya kuelekea nchini Saudi Arabia.

Nawaz Sharif ambaye aling’olewa madarakani na mshirika wa karibu wa Marekani rais Musharaf katika mapinduzi yaliyofanyika bila umwagikaji damu mwaka 1999 aliahidi kwamba kurudi kwake Pakistan kungetoa msukumo wa mwisho dhidi ya utawala wa kidekteta wa rais Musharaf ambaye anakabiliwa na mzozo wa hali ya juu tangu aingie madarakani.

Hii inatokana na wimbi la mivutano ya kisiasa pamoja na ghasia za wenye msimamo mkali wa kidini.

Ijaz ul Haq waziri anayehusika na masuala ya dini nchini Pakistan amesema Wasaudi walitamka wazi kwamba wanataka arudi nchini Saudi Arabia na kwa hivyo sio tu ameiabisha Pakistan lakini hata uongozi wa Saudi Arabia kwa kukiuka makubaliano.

Itakumbukwa kwamba baada ya kung’olewa madarakani mwaka 1999 Sharif alihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kukutikana na hatia ya kukwepa kulipa kodi na makosa ya uhaini lakini mwezi Desemba mwaka 2000 aliachiwa huru kwa sharti kwamba yeye pamoja na familia yake watakwenda kuishi uhamishoni nchini Saudi Arabia kwa miaka 10.Lakini mahakama kuu ilipitisha uamuzi mwezi uliopita kwamba anaweza kurudi nyumbani.Jambo ambalo limeonyesha kuna hali ya kutofautiana kati ya mahakama na Musharaf tangu alipojaribu kumfuta kazi mwanasheria mkuu Iftikhar Muhammed Chaudhry mapema mwaka huu.

Hata hivyo Sharif sasa amekubali kubakia nchini Saudi Arabia hadi mwaka 2010 kama ilivyofikiwa katika makubaliano ambayo yalimfanya aachiwe huru kutoka jela.

Ukizungumzia mzozo wa Pakistan Umoja wa Ulaya umeitolea serikali ya Pakistan kuheshimu uamuzi wa mahakama kuu ukisema Sharif anapaswa kupewa nafasi ya kujitetea katika mahakama nchini Pakistan.

Marekani kupitia msemaji wa ikulu imesema kurudishwa kwa Sharif ni suala la ndani ya Pakistan lakini imekumbusha kwamba uchaguzi ujao lazima ufanyike kwa njia iliyo huru nay a haki.

Mapema asubihi ya Leo wafuasi wa Nawaz Sharif walionekana katika uwanja wa ndege wakiimba nenda Musharaf nenda na maisha marefu kwa Nawaz Sharif.Polisi walikabiliana na kiasi cha watu 100 wafuasi wa Sharif pamoja na kuwakamata wanachama wakuu wa chama chake cha Muslim League.Wafuasi wengine watano wa Sharif walijeruhiwa katika mashambuliano ya risasi na Polisi huko kaskazini mashariki mwa Pakistan.

Nduguye Sharif ambaye alikuwa amepanga kusafiri pamoja naye kutoka nchini Uingereza lakini akaghairi dakika za mwisho amesema Sharif atajaribu tena kurudi nyumbani hivi karibuni.