1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Afrika zahimizwa kumbinya Mugabe ajiuzulu

23 Machi 2007

Serikali ya Zimbabwe imekanusha taarifa zinazosema kuwa Angola ina mpango wa kuwapeleka askari wake 3000 kukisaidia kikosi cha polisi nchini Zimbamwe, nchi hiyo imesema kuwa ina uwezo wa kutosha kushughulikia maswala yake ya usalama.

https://p.dw.com/p/CHHf

Waziri wa mambo ya ndani wa Zimbabwe Kembo Mohadi amesema kuwa habari hizo ni uzushi mtupu na wala Zimbabwe haihitaji msaada kutoka nje.

Gazeti la Times la mjini London lilinukuu tarifa iliyotaja kuwa takriban askari 2,500 wa Angola watapelekwa huko nchini Zimbabwe kukisaidia kikosi cha usalama cha rais Robert Mugabe.

Ubalozi wa Angola mjini Harare pia umekanusha vikali taarifa hizo na kuongeza kuwa sio desturi ya Angola kuingilia maswala ya ndani ya nchi zingine.

Ubalozi wa Angola nchini Zimbabwe umeeleza madhumuni ya ziara ya waziri wake wa mambo ya ndani ilikuwa ni kutia saini mkataba wa maelewano baina ya nchi hizo mbili.

Angola na Zimbabwe ni wanachama wa SADC na nchi hizo zina uhusiano wa kisiasa licha ya jumuiya ya kimataifa kushutumu hali ya kisiasa na kiuchumi inayoendela kuzorota nchini Zimbabwe chini ya utawala wa rais Robert Mugabe mwenye umri wa miaka 83 na aliyeiongoza nchi hiyo tangu ilipopata uhuru wake mwaka 1980.

Wakati huo huo waziri mkuu wa Australia John Howard amezitaka nchi jirani za Zimbabwe kumbinya rais Mugabe ili ajiuzulu.

Bwana Howard amesema amechoshwa na msimao wa nchi kama Afrika Kusini ambayo inasema kuwa Zimbabwe iachwe itaue yenyewe mzozo wake wa ndani.

Waziri mkuu huyo wa Australia ameulaumu utawala wa rais Mugabe na kwamba nchi hiyo ni miongoni mwa nchi zenye hali duni ya maisha kwa raia wake, kiwango cha matumizi kimepanda sana na pia inasifa ya kuwakandamiza wapinzani.

Matukio ya hivi karibuni ya kupigwa wanachama wa upinzani nchini Zimbabwe yametoa nafasi kwa bara ulaya kuanza kuukodolea macho mzozo wa kibinadamu na kiuchumu nchini Zimbabwe, hayo ni kwa mujibu wa mwanachama mmoja wa chama cha upinzani cha MDC David Coltart.

Amesema si hayo tu bali hata umoja wa Afrika umeanza kupaaza sauti juu ya kuzorota kwa nchi ya Zimbabwe ambayo awali ilifahamika kwa uchumi wake mzuri na jinsi inavyoanza kuwa mzigo kwa nchi zingine za Afrika.

Coltart akizungumza na shirika la habari la Reuters ameutaka umoja wa ulaya kumteuwa mjumbe kama vile mkuu wa sera za nje za umoja wa ulaya Javier Solana kushirikiana na majirani wa Zimbabwe kama Afrika Kusini, Msumbiji, Botswana na Zambia kutafuta suluhisho katika mzozo unaoikumba Zimbabwe.

Gharama za maisha nchini Zimbabwe zimepanda kwa zaidi ya asilimia 1,700 na ukosefu wa ajira umefikia asilimia 80, nchi hiyo pia inakumbwa na uhaba wa chakula na mafuta.

Tangu mgogoro wa nchi hiyo uanze mwaka 2000 kufuatia kunyang’anywa mashamba wakulima wa kizungu viongozi wa nchi za Afrika Kusini wamekuwa wakinyamaa kimya, lakini kufuatia kupigwa kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai na wenzanke na wengineo kunyimwa ruhusa ya kutoka nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, nchi jirani zimeanza kubadili msimao wake, kwani Zimbabwe kutumbukia katika mzozo italeta mtafaruku katika eneo zima la Afrika.