1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Afrika zamtaka Trump kuomba radhi

Caro Robi
13 Januari 2018

Nchi zote 54 za Afrika katika Umoja wa Mataifa zimemtaka Rais wa Marekani Donald Trump kuziomba radhi baada ya kuripotiwa kutumia maneno machafu alipokuwa akizungumzia kuhusu wahamiaji kutoka Afrika, Haiti na Salvador.

https://p.dw.com/p/2qn3o
US-Präsident Donald Trump
Picha: picture-alliance/abaca/O. Douliery

Baada ya kikao cha dharura cha mabalozi wa nchi za Afrika katika Umoja wa Mataifa, mabalozi hao wamesema wanatiwa wasiwasi na mtindo unaozidi kujitokeza kutoka utawala wa Marekani wa kuwadunisha Waafrika na bara la Afrika na kulaani vikali matamshi ya kibaguzi, ya kudunisha na ya chuki dhidi ya wageni yaliyotolewa na Rais Trump.

Mabalozi hao pia wamewashukuru Wamarekani wa tabaka mbali mbali waliolaani matamshi ya Trump. Kauli ya Trump imesababisha ghadhabu na mshtuko. Umoja wa Afrika umemshutumu Trump kwa matamshi yake ukisema umeshtushwa na umesikitishwa na Rais Trump na umemtaka aombe radhi.

Ebba Kalondo, msemaji wa Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Moussa Faki amesema matamshi ya Rais huyo wa Marekani yanakiuka tabia zinazokubalika na za kiungwana.

Äthiopien 29. African Union Summit in Addis Abeba
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Moussa FakiPicha: picture-alliance/abaca/M. Wondimu Hailu

Nchi za Botswana na Senegal zimewaita mabalozi wa Marekani katika nchi hizo kulalamika kuhusu kauli chafu za Trump na pia kupata ufafanuzi iwapo nchi hizo ni miongoni mwa zinazochukuliwa kuwa zilizooza. Umoja wa Mataifa pia umelaani matamshi ya kiongozi huyo wa Marekani.

Rais Donald Trump amekanusha kutumia maneno machafu juu ya nchi kadhaa ikiwa pamoja na za Afrika, akijitetea kwa kusema alikuwa tu akielezea kile watu wengi wanafikiria lakinii hawadiriki kusema kuhusu wahamiaji kutoka nchi masikini.

Kulingana na mmoja wa washirika wake wa karibu ambaye jina lake halikutajwa kwasababu haruhusiwi kuzungumza na vyombo vya habari, amesema rais huyo hajutii kauli yake hiyo ya kuziita nchi za Afrika na nyinginezo zilizooza, akikanusha kuwa ni mbaguzi na badala yake akivilaumu vyombo vya habari kwa kupotosha maana ya kauli yake.

Trump ameshutumiwa vikali na Wamarekani wa tabaka mbali mbalii wakiwemo wanasiasa wa chama cha Democrat na hata wa chama chake cha Republican. Seneta John McCain amesema viongozi wote waliochaguliwa akiwemo Rais wanapaswa kuwaheshimu watu kutoka kila pembe ya dunia ambao amesema wameifanya Marekani kuwa imara tena.

USA Trump erhöht den Druck auf den Iran
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: picture alliance/dpa/AP/E. Vucci

Spika wa bunge la Marekani Paul Ryan amesema matamshi ya matusi ya Trump kuhusu Afrika ni ya kusikitisha na si ya tija.

Inaripotiwa siku ya Alhamisi wiki hii, Trump alipokutana na wabunge kadhaa katika Ikulu ya Rais ya White House kujadili mageuzi ya sheria ya uhamiaji aliuliza kwa nini Marekani iwapokee wahamiaji kutoka nchi za uozo kama za Afrika, Haiti na El Salvador badala ya kuwapokea wahamiaji kutoka nchi kama Norway.

Haiti na El Savador pia zimelaani vikali kauli chafu ya kibaguzi aliyoitoa Trump. Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imejikuta na kibarua cha kujaribu kutuliza mambo baada ya Trump kuibua ghadhabu Afrika, Haiti na El Savador.

Mwandishi: Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Zainab Aziz