1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUbelgiji

Nchi za EU zaafikiana kuhusu mkataba wa wahamiaji

4 Oktoba 2023

Mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya yamekubaliana kuhusu marekebisho ya mwisho ya sheria za jinsi ya kuwashughulikia wahamiaji wanaofika katika nchi za umoja huo bila vibali wakitafuta hifadhi.

https://p.dw.com/p/4X6rx
Mageuzi yanalenga kuziondolea mzigo nchi ambazo wahamiaji hufika mwanzo kama Italia na Ugiriki kwa kuwawezesha kuwahamisha wahamiaji hadi mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya.
Mageuzi yanalenga kuziondolea mzigo nchi ambazo wahamiaji hufika mwanzo kama Italia na Ugiriki kwa kuwawezesha kuwahamisha wahamiaji hadi mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya.Picha: Cecilia Fabiano/AP Photo/picture alliance

Hatua hiyo inayasogeza mbele makubaliano hayo ili yawe sheria ifikapo mwaka ujao. 

Wajumbe wa nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya wamefikia makubaliano hayo mjini Brussels Ubelgiji, dakika za mwisho baada ya Ujerumani na Italia kusuluhisha mzozo kati yao kuhusu mashirika ya misaada yanayowaokoa wahamiaji katika Bahari ya Mediterrania.

Lengo la Umoja wa Ulaya ni kuhakikisha mageuzi yaliyokwama yanawekwa kuwa sheria kabla ya uchaguzi ujao wa bunge la Ulaya na wa halmashauri yake kuu.

Margaritis Schinas ambaye ni makamu wa rais wa Halmashauri kuu ya umoja huo amesema hatua hiyo inawaweka katika nafasi nzuri na bunge la Ulaya kufikia makubaliano juu ya mkataba mzima wa uhamiaji na uombaji hifadhi ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Mkuu wa Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ameyakaribisha makubaliano yaliyofikiwa na nchi wanachama kuhusu mageuzi ya uhamiaji na uombaji hifadhi.
Mkuu wa Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ameyakaribisha makubaliano yaliyofikiwa na nchi wanachama kuhusu mageuzi ya uhamiaji na uombaji hifadhi.Picha: Jean-Francois Badias/AP Photo/picture alliance

Mataifa ya EU yajaribu kupata makubaliano kuhusu wahamiaji

Schinas aliyataja makubaliano hayo kama kiungo cha mwisho kilichokosekana kwenye mchakato huo” na ameyahimiza mataifa ya Umoja wa Ulaya pamoja na bunge la Ulaya kuendeleza mazungumzo na makubaliano hayo na kutunga sheria haraka, akihoji muda haupo wa kupoteza.

Kutokana na kuongezeka kwa vyama vya mrengo wa kulia katika nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya, na vilevile uwezo wa Hungary na Poland kushika nafasi ya urais wa Umoja wa Ulaya kwa zamu, huenda kukawa na mabadiliko kwenye siasa za Umoja Ulaya.

Nchi ambako wahamiaji hufika mwanzo kuruhusiwa kuwahamisha hadi mataifa mengine ya EU

Punde itakapotekelezwa, mkataba mpya wa Uhamiaji na Uhifadhi utaziruhusu nchi ambazo wahamiaji huwasili kwanza kama Italia na Ugiriki, kuwahamisha hadi mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya na hivyo kuziondolea mzigo huo.

Usafirishaji haramu wa binaadamu watishia watoto wa Afrika

Nchi ambazo zinapinga kuwahifadhi wahamiaji kama Poland na Hungary zitalazimika kulipa kiwango cha fedha kwa nchi nyingine zinazowapokea wahamiaji.

Mataifa tajiri yanawahitaji sana wahamiaji , asema mkuu wa IOM

Aidha Umoja wa Ulaya utaharakisha mchakato wa kutathmini waomba hifadhi ili wasiohitimu viwango vya kupewa hifadhi, waweze kurudishwa katika mataifa walikotoka kabla ya kufika Ulaya. Isitoshe muda wa kuwashikilia wahamiaji mpakani pia unaweza kurefushwa zaidi kuliko muda wa sasa wa wiki 12.

Mkwamo kuhusu suala hilo ulizusha wasiwasi kwenye umoja huo mnamo wakati unakabiliwa na ongezeko la wahamiaji wanaowasili kinyume cha sheria.

Sehemu ya lengo la sera hiyo iliyorekebishwa ni kwa nchi za Umoja wa Ulaya kuchukua hatua kwa pamoja iwapo zitakabiliwa na ongezeko kubwa la waomba hifadhi, kama ilivyotokea mwaka 2015-2016 wakati mamia ya maelfu ya wahamiaji walipowasili.

Chanzo: (AFPE)