1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Kiarabu zajadili mpango wa amani ya mashariki ya kati

Saumu Mwasimba30 Julai 2007

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za kiarabu wameanza mkutano wao juu ya kuufufua mpango wa amani ya mashariki ya kati.

https://p.dw.com/p/CHAK
Picha: AP

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 16 wanachama wa umoja wa nchi za kiarabu wamekutana makao makuu ya umoja huo mjini Cairo Misri kuzungumzia juu ya kuufufua mpango wa amani wa mashariki kati.

Mkutano huo unazingatia juhudi za amani za mataifa ya kiarabu pamoja na pendekezo la rais Gorge w Bush wa Marekani wa kutaka pafanyike mkutano juu ya mpango wa amani mashariki ya kati katika msimu wa mapukutiko mwaka ujao.

Kabla ya kuanza kikao cha leo katibu mkuu wa umoja huo Amr Mussa alisema umoja huo unalichukulia kwa uzito mkubwa suala la kuufufua mpango wa amani ya mashariki ya kati na kubadili hali ya sasa kwenye eneo hilo na kwahivyo hawako tayari kujitumbukiza kwenye mpango ambao hautafanikiwa.

Kikao cha leo pia kitasikiliza ripoti ya waziri wa mambo ya nje wa Misri Ahmed Abul Gheit ambaye wiki iliyopita alikwenda Israel na kudokeza kwamba nchi hiyo imeupokea vyema mpango wa amani wa nchi za kiarabu na kuahidi kurejesha uhusiano wa kawaida na nchi hizo kwa kuwapa wapalestina dola lao na kuondoka kwenye ardhi walioinyakua tangu mwaka 1967 pamoja na suala la kurudi wakimbizi wakipalestina walioko nje ya Palestina.

Mpango huo ulipendekezwa mara ya kwanza katika mkutano wa kilele wa nchi za kiarabu nchini Lebanon mwaka 2002 na kusisitizwa nchini Saudi Arabia mwaka huu lakini Israel ilionekana kupinga suala la kurudi wakimbizi wa kipalestina.

Palestina kwa sasa imegawika zaidi tangu Hamas ichukue udhibiti wa eneo la ukanda wa Gaza huku serikali iliyokuwa ikiongozwa na kundi hilo ikiondolea na kuundwa serikali mpya ya dharura iliyona makao yake ukingo wa magharibi.

Mbali na kujadili juu ya hali hiyo kikao cha mjini Cairo pia kinatazamiwa kuzungumzia suala la Libya baada ya Bulgaria kuwasamehe wataalamu wake sita wa matibabu walioachiliwa nchini Libya ambako walikuwa wakitumikia kifungo cha maisha kufuatia tuhuma za kuhusika na uambukizaji watoto virusi vya HIV.

Hoja hiyo huenda ikazungumza licha ya Libya ambayo haishirikia kikao cha leo kupinga agenda hiyo kwenye mkutano huo.