1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

110209 Israel Reaktionen

Aboubakary Jumaa Liongo12 Februari 2009

Wakati Tzipi Livni na Benjamin Netanyahu wakiendelea kuwa wakakamavu wa kudai kushinda uchaguzi mkuu wa Israel, vyombo vya habari katika nchi za kiarabu vimeubeza na kutoonesha matumaini yoyote kwa matokeo ya uchaguzi

https://p.dw.com/p/GsIN
Bango linaloonesha picha za Nentanyahu na Bi LivniPicha: AP

Chama cha Kadima kinachoongozwa na Tzipi Livni kimepata viti 28 huku kile cha Likud cha Benjamin Netanyahu kimepata viti 27 lakini washirika wake wa mrengo wa kulia wamepata viti vingi, na hivyo kumpa nafasi nzuri ya kuunda serikali.

Hata hivyo kwa nchi za kiarabu hakuna matokeo hayo hayakuleta matumaini , kama vinavyosema vyombo vya habari vya nchi hizo.


Jee maoni katika mataifa ya kiarabu juu ya matokeo ya uchaguzi wa Israel yakoje ?Kutoka Amman Jordan

Gazeti la Al-Ahram la nchini Misri likiandika juu ya uhaguzi huo, limejiuliza inawezakana vipi kwa jamii inayokabiliwa na njaa ya amani kumuunga mkono kwa kiasi kikubwa mtu kama Lieberman mwenye sera za kifashisti?


Waarabu wengi wanayachukulia matokeo ya uchaguzi huo kuwa yasiyo na matumaini yoyote.Wanaamini ya kwamba tofauti zilipo kati vyama vikuu vya Israel Kadima na Likud si kubwa wakitolea mfano wa vita vya Ukanda wa Gaza ambavyo viliongozwa na Waziri wa Ulinzi Ehud Barak kutoka chama cha mrengo wa shoto cha Leba kinachoshirikina na Kadima kuunda serikali ya sasa.


Baria Alamuddin ni mwandishi wa habari wa gazeti la Al Hayat ambaye anasema hamna tofauti kati ya Tzipi Livni na Benjamin Netanyahu.

´´Suala ni nani ataunda serikali, kwasababu sote tunaweza kuona, kwamba jinsi hali inavyokwenda inaelekea upande wa mrengo wa kulia.Na hii itazidisha misimamo ya siasa kali na zaidi za kidini upande wa Israel na bilashaka nao pia watakabiliana na hali hiyo hiyo. Siasa kali zinaota mizizi pande zote mbili, hii ni kutokana na kukosekana kwa amani´´


Kwa upande wake gazeti la Al-Rai la Jordan linasema kuwa mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel dhidi ya Wapalestina hayakuweza kufikia lengo la kupata usalama au amani, kwa hivyo gazeti hilo linaongeza kuwa ni vyema kwa Israel kufahamu ya kwamba sera za kuwaua Wapalestina hazijaleta maendeleo na mafanikio yoyote.

Gazeti hilo limeendelea kuandika kwa kusema kuwa bado kuna nafasi ya kupatikana amani katika eneo hilo na kwamba pendekezo la kuwepo kwa mataifa mawili ndiyo suluhisho.Linamalizia kwa kusema kuwa hivi sasa ni juu ya Israel kuamua kuelewa maana ya amani au kuendelea na vitendo vyake vya kijeuri.

Naye mwandishi wa habari Dalal al-Bizri katika makala yake ameandika kwamba Israel imejitumbukiza zaidi katika mzozo.Haiwezi kutatua suala la ardhi kwa njia ya amani na hivyo kurudisha nyuma zaidi upatikanaji wa amani.


Mwandishi huyo anasema kuwa Israel haina tena matumaini ya kuwepo amani, kwahivyo imekuwa ikiendelea kufanya mashambulizi mara kwa mara.


Mwandishi huyo al-Bizri lakini pia anaona ya kwamba Waarabu nao pia wako katika hali kama hiyo, tukimnukuu anasema ´´kadri tunavyoendelea kupigana ndiyo tunatoa nafasi kwa mahafidhina kuzidi kuathiri ajenda na mtizamo wetu kisiasa´´ mwisho wa kumnukuu.


Waarabu bado wanakumbuka jinsi serikali ya mwanzo ya Benjamin Netanyahu katika miaka ya themanini ambapo wanamuona kama mtu aliyekuwa na mpango wa amani kwa njia ya kuweza vizuizi.

Kitu muhimu kwa waarabu anasema mwandishi huyo, si nani atakayekuwa Waziri Mkuu wa Israel, lakini muhimu ni njia gani kiongozi huyo atatumia kuongoza.

Juhudi za nchi za kiarabu za kuwepo amani na Israel zilizoanza mwaka 2002 bado ziko mezani, ambazo zinaitaka Israel iondoke kutoka katika ardhi inazokalia, kuwepo kwa mataifa mawili ya Israel na Palestina , pamoja na utatuzi wa suala la wakimbizi wa kipalestina.


Mpaka sasa Israel haijaupokea mkono wa mapendekezo hayo uliyonyooshwa na nchi za kiarabu.

Serikali za Kiarabu hivi sasa zinatumaini ya kwamba Israel itaacha ukaidi wake wa kukaata kukubaliana na mapendekezo hayo.


Wakati huo huo Serikali ya Jordan imesema kuwa inamatumani serikali mpya itakayoundwa nchini Israel itatilia maanani suala la mpango wa amani Mashariki ya Kati na kwamba itajiandaa kuingia katika majadiliano na wapalestina yatakayozaa matunda.


Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan Salah Bashir pia amesema kuwa serikali yoyote itakayoundwa ni lazima iazimie kusitisha ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi huko Mashariki mwa Jerusalem.


Amesema kuwa Israel na Palestina ni lazima zifanye mazungumzo ya amani yenye mtizamo wa kufikia makubaliano kamili ya kuwepo kwa mataifa mawili Israel na Palestina kama suluhisho la mzozo huo.