1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za kiarabu zitakwenda Annapolis

Oummilkheir23 Novemba 2007

Matumaini mema kwa mkutano wa kimataifa wa mashariki ya kati

https://p.dw.com/p/CSSF
Annapolis, utakakofanyika mkutano wa Mashariki ya katiPicha: DW

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa jumuia ya nchi za kiarabu waliokua wakikutana mjini Cairo Misri,wameamua kushiriki katika mkutano wa kimataifa wa Annapolis Marekani kuhusu amani ya mashariki ya kati.

“Nchi za kiarabu zinazokutana Cairo zimekubali mwaliko wa kushiriki katika mkutano wa Annapolis kwa daraja ya mawaziri”-taarifa iliyochapishwa mwishoni mwa mkutano huo wa Cairo imesema.

Taarifa hiyo haikuitaja kinaga ubaga Syria ambayo waziri wake wa mambo ya nchi za nje Walid Mouallem alisema hapo awali Damascus haitoshiriki katika mkutano wa kimataifa ikiwa Washington haitoingiza suala la milima ya Golan inayokaliwa na Israel katika ajenda ya mazungumzo.

“Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani bibi Condoleezza Rice ameahidi jibu la maana na tukilipata basi Syria itahudhuria mkutano wa Annapolis” alisema bwana walid Mouallem wakati wa mkutano pamoja na waandishi habari mjini Cairo.

Syria inashikilia irejeshewe eneo lote la milima ya Golan iliyotekwa mwaka 1967 na Israel na kudhibitiwa baadae mwaka 1981.Mazungumzo ya amani kati ya Israel na Syria yamekwama tangu mwaka 2000.

October mwaka huu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleeza Rice aliondowa uwezekano wa kujumuimshwa suala laq milima ya Golan katika ajenda ya mazungumzo ya Annapolis,kabla ya kukiri “ili kupata uungaji mkono mkubwa wa nchi za kiarabu,Marekani itabidi iingize masuala mengine pia ya mzozo wa mashariki ya kati.

Kwa upande wake katibu mkuu wa jumuia ya nchi za kiarabu Amr Moussa amesema hii leo Saud Arabia,ambayo sawa na nchi nyengine za kiarabu ilikua ikijiuliza kama ishiriki au la ikihofia mkutano wa Annapolisi usije ukamalizika bila ya tija,imeamua kushiriki na itawakilishwa na waziri wa mambo ya nchi za nje Saoud el Faysal.

Uamuzi wa nchi za kiarabu wa kushiriki katika mkutano wa Annapolis unaimarisha msimamo wa kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas na kumuwezesha wakati huo huo waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert atambe na kuitanabahisha jamii ya waisrael kuhusu uwezekano wa kupatikana amani pamoja na waarabu.

Israel imesifu uamuzi wa nchi za kiarabu wa kushiriki katika mazungumzo ya Annapolis na kuutaja uamuzi huo kua ni “hatua ya maana na muhimu.”

“Tunaamini kushiriki mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi za kiarabu katika mkutano wa Annapolis ni hatua muhimu inayoweza kufungua njia ya kufanikiwa juhudi hizo”-Amesema msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Israel Mark Regev..

Matamshi kama hayo yametolewa pia na msemaji wa waziri mkuu wa Israel Miri Eisin.

Kinyume na hayo,wafuasi wa Hamas,walioahidi kuitisha mkutano wao Gaza jumatattu ijayo kupinga ule wa Annapolis,wamewataka viongozi wan chi za kiarabu wasianzishe uhusiano pamoja na Israel.

Kabla ya mkutano wa Cairo,Misri,Jordan,nchi mbili pekee za kiatabu zilizotiliana saini makubaliano ya amani pamoja na Israel zilisema zitahudhuria mkutano wa Annapolis.Rais Hosni Mubarak na mfalme Abdallah wa pili wa Jordawn walifika hadi ya kuzungumzia “matumaini mema” kuelekea mkutano huo.

“Mkutano wa Annapolis unaweza kuondowa kiu cha wapalastina na ulimwengu wa kiarabu pamoja na wote wanaofuatilizia utaratibu wa amani”alisema hapo awali msemaji wa rais wa Misri Suleiman Awad.

Falme ya Oman nayo pia imetangaza rasmi kushiriki katika mkutano wa Annapolis.