1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NCHI ZA NILE BASIN INITIATIVE ZASONGA MBELE NA MIRADI ENDELEVU

30 Januari 2007

Miradi ya umeme imepewa kipaumbele

https://p.dw.com/p/CHli

Uamuzi wa nchi 10 zinazozunguka bonde la Mto Nile kuwa na mradi wa pamoja wa nguvu za umeme ili kukabiliana na upungufu mkubwa wa umeme ambao umekuwa ukijitokeza mara kwa mara niwa kutia moyo endapo lakini utafanikiwa.

Ili kufanikisha azma hiyo umoja huu umeunda taasisi itakayoshughulikia mradi huu ambayo imebatizwa jina la Nile Basin Power Forum ambayo imeisha tangaza mikakati yake ya kutayarisha kituo cha pamoja cha umeme power pool na kutayarisha uchambuzi yakinifu wa namna ya kuunganisha nyaya za umeme kutoka nchi moja kwenda nyingine miongoni mwa nchi wanachama.

Mpango huu wa kuhakikisha nchi hizi zinapata umeme wa kutosha kwa wakati wote ni moja ya miradi ya umoja wa nchi hizi 10 zinazojulikana kama Nile Basin Initiative (NBI).

Nchi hizi ni Kenya Tanzania Uganda Rwanda Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC Ethiopia, Sudan Misri na Eritrea.

Mwanzoni mwa mwaka huu nchi hizi zilikutana katika mji wa kitalii wa Bagamoyo nchini Tanzania ulio umbali wa kilometa zipatazo 70 kutoka mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania Dar es salaam ili kudurusu mafanikio ya miradi 12 inayopaniwa na NBI.

Kama ilivyo kawaida mkutano huu ulihudhuriwa na mawaziri wa maji kutoka nchi hizi. Lengo hasa la mkutano huo lilikuwa kutoa maelekezo ya kisera kwa ajiri ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Wenyewe mawaziri waliwaambia waandishi wa habari mjini Bagamoyo kuwa miradi hii ilianzishwa ili kudumisha ushirikiano katika kutunza vyanzo mbalimbali vya maji, ambayo huenda mto Nile na katika maziwa ambayo yanaleta maji mto Nile.

Sio tu kutunza bali pia katika kutafuta njia mwafaka za ugawanaji na kwa usawa, rasilimali zinazopatikana kutokana na mito na maziwa yaliyo katika eneo hili.

Ikumbukwe kuwa watu wapatao milioni 90 wanalitegemea bonde hili la mto Nile wenye urefu wa maili 4,160. Zaidi ya hayo watu milioni 300 hunufaika kutokana na rasilmali za bonde hili.

Dk. Shukuru Kawambwa ni waziri wa maji wa Tanzania. Ndiye alikuwa waziri mwenyeji katika mkutano huu. Aliiambia Deutsche Welle kuwa miradi 12 iliyoanzishwa na umoja huu inaendelea kusimamiwa na kuendeshwa aidha katika nchi mbili, nchi tatu, hadi nne za umoja huu.

“Ni miradi ya kuendeleza bonde la mto nile na kuendeleza mali ya asili ya maji katika bonde hilo la mto Nile. Kipindi hiki ambapo tunakutana sisi kama mawaziri wa Maziwa Makuu katika bonde la Nile ni kipindi muhimu sana kwa sababu kinatuelekeza katika taratibu za makubaliano ya ushirikiano wa matumizi ya maji na usalama wa maji katika bonde la mto nile yaani kwa nchi 10”, anabainisha waziri Kawambwa.

Katika mkutano huu kwa hiyo licha ya kudurusu miradi yote hii, mradi wa umeme ulipewa kipaumbele.

“Nishati ni suala kubwa na ni suala muhimu kwa nchi zetu zote ili kupiga hatua za maendeleo ni muhimu sana kwamba kuwe na nishati”, anaongeza waziri Kawambwa.

Mkutano huu kwa upande mwingine ulilenga kuwavutia wafadhili mbalimbali na mashirika ya kimataifa maana walikaribishwa hata wawakilishi wa mashirika hayo au mabalozi wanao ziwakilisha nchi zao Tanzania.

Moja ya miradi ya umeme ambao umezingatiwa sana katika mkutano huu ni ule wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rusumo ulio mpakani mwa Tanzania na Rwanda.

Wataalamu wa masuala ya umeme wanasema mradi huu ukifanikiwa utaweza kuzalisha hadi megawati 60, zitakazotumiwa na nchi hizi majirani, yaani Rwanda, Tanzania na hata Burundi na Uganda.

Tayari mradi huu umefanyiwa upembuzi yakinifu.

“ni moja kati ya miradi ambayo tunaipa kipaumbele sana kwa hiyo MUNGU akijalia kupata funding na pia fedha zetu wenyewe katika ushirikiano wa nchi hizi…..tunatarajia kuzalisha nguvu za umeme katika maporomoko hayo” waziri Kawambwa aliithibitishia Deutsche Welle.

Anasema lakini kuwa hakuna kikubwa kilichofanyika hadi sasa mbali na upembuzi yakinifu lakini anadokeza kuwa umoja huu una matumaini makubwa kuwa mradi huu utakubaliwa na kupata wafadhili.

Kuonyesha jinsi mradi wa umeme katika nchi hizi ulivyopewa mazingatio makubwa wataalam wa kutoka nchi hizi wanaohusika na mausala ya umeme walikutana tena katika hoteli ya White sands jijini Dar es salaam na kuweka mikakati mipya ya kuusukuma mbele mpango huu.

Pamoja na kwamba nchi hizi 10 zipo kwenye mwavuli mmoja wa NBI zimegawanywa katika makundi mawili. Kundi moja linajulikana kama Nile Equatorial Lakes Subsidiary Action Program NELSAP na lingine Eastern Nile Subsidiary Action Program ENSAP.

NELSAP ni nchi za Kenya, Rwanda, Misri, Sudan, Tanzania, na Uganda wakati ENSAP ni Ethiopia, Misri, na Sudan. Katika mradi huu Eritrea inabaki kama mtazamaji observer.

Kwa hiyo mkutano wa mwaka huu ulikusudia hasa kuangalia mafanikio ya NELSAP, na mikakati mipya inayopewa kipaumbele na jumuia hii.

Miradi ya NELSAP kwa kiasi kikubwa inafadhiliwa na Benki ya Dunia, SIDA Sweden, CIDA Canada, Umoja wa Ulaya, Benki ya maendeleo ya Afrika ADB, na Netherlands.

Kuna pia kamati maalumu ya wataalamu inayofanya uchambuzi na ufuatiliaji wa miradi hii Nile Technical Advisory Committee, hii ilikutana siku tatu kabla ya kuanza mkutano wa mawaziri hawa.

NELSAP inaendesha miradi hii ikiwa imeitenga katika makundi makubwa mawili ambayo ni Miradi ya Umeme na maendeleo ya mali za asili zilizo katika nchi za umoja huu.

Ile inayoendeleza mali ya asili ni kama ile ya ziwa Edward na Albert ya uvuvi inayoendeshwa na kuzinufaisha nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na Uganda. Miradi mingine ni Mara- Sio – Malakisi. .

Ya umeme kama nilivyotangulia kutaja ni kama ule wa Regional Rusumo Falls Hydroelectric and Multipurpose Project RRFP ambao uliidhinishwa April 2005 na mawaziri wa nishati kutoka nchi za Rwanda Burundi na Tanzania.

Mradi mwingine ni wa Mara River Basin Management unaoendeshwa na nchi za Kenya na Tanzania. Ule wa Sio-Malaba-Malakisi river Basin unazishiriksiha nchi za Uganda na Kenya.

Hii ni pamoja na mradi endelevu ambao umeanza siku nyingi kidogo wa Uhifadhi maji ya ziwa Victoria ujulikanao kama LVEMP 11 ambao unasimamiwa na nchi zinazozunguka Ziwa Victoria yaani Kenya Tanzania na Uganda.

Akifungua mkutano huo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Edward Lowassa alisema mkutano huo umefanyika katika wakati ambapo Tanzania na baadhi ya nchi majirani zimeshuhudia misiba ya kimaumbile kama vile mafuriko na ukame.

Anasema misiba hiyo imepelekea kuwepo matatizo ya chakula na ukosefu wa usalama kwa baadhi ya maeneo, lakini zaidi matatizo ya umeme ambayo yamepelekea viwanda vingi kutofanya kazi za uzalishaji kwa kiwango kinachotakikana.

Waziri Mkuu anasema matokeo yake ukuaji wa uchumi nchini Tanzania utapungua kutoka asilimia 6.8 zilizofikiwa hadi mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 5.9 kwa mwaka 2006.

Mradi mwingine unaosimamiwa na nchi katika makundi ni ule unaoendeshwa na serikali za Kenya na Uganda na kuzinufaisha wilaya nane za nchi hizo ambazo ni Busia, Tororo, Manafwa na Mbale, za Uganda. Pia Busia, Bungoma, Mt. Elgon na Teso ambazo ni za Kenya.

Kwa upande wake ENSAP nayo inaendeleza juhudi kama hizi katika kilimo cha umwagiliaji kama vile Misri lakini pia katika kuzalisha umeme.

Kwa mfano inadhaniwa kuwa ikiendeleza rasilimali ilizonazo katika kuzalisha umeme Ethiopia inaweza kuzalisha hadi mw 45,000 wakati Sudan na Misri zina rasilimlai za gesi na mafuta ambayo inaweza kuzalisha umeme kwa kiwango kikubwa vile vile.

Mradi huu ukifanikiwa wa kuunganisha mtandao wa umeme katika nchi hizi, wanadai wataalamu hakutakuwepo na uhaba wa umeme hata kama yatajitokeza mabadiliko makubwa ya hali ya hewa kama ambayo yamekuwa yakijitokeza.

Hii ni kutokana na mantiki kuwa wakati kuna mvua ya kutosha nchi zile zinazozalisha umeme utokanao na nguvu ya maji Hydro power, zitazalisha umeme wa kutosha na utatumiwa na nchi zote na wakati wa hali au ukame basi nchi zote zitatumia umeme unaozalisha na nchi zinazozalisha umeme kutokana na mafuta.

Hivi sasa Sudan inazalisha jumla ya Megawati 917 wakati Ethiopia inazalisha jumla ya mw 747. lakini nchi hizi zimejiwekea malengo ya kuzalisha kiasi kukubwa cha umeme.

Mfano Sudani inataka ifikapo mwaka 2010 izalishe mw 3191 mwaka 2014 izalishe mw 4929 na mwaka 2025 izalishe mw 6337.

Vivyo hivyo na Ethiopia nayo inataka ifikapo mwaka 2010 izalishe mw 1301, mwaka 2013 mw 1993, na mwaka 2025 ifikie mw 5797.

Lakini mbinu hii kwa upande mwingine itazinufaisha nchi za NBI kwa kuwa baadhi ya nchi katika umoja huu kama vile Misri tayari imejiunga kwenye mtandao wa umeme kutoka baadhi ya mataifa mengine ya kiarabu ambayo baadhi yamejiunga na mtandao wa umeme wa nchi za bara la Ulaya.

Mkakati huu kwa upande mwingine unafanana sana na ule wa Southern African Power Pool kwa ufupi SAPP.

SAPP ni mradi wa nchi zilizo kwenye SADC ambayo baadhi yake kama vile Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, zimo kwenye kwenye NBI lakini pia ni nchi wanachama katika SADC.

Makao makuu SAPP ni Afrika Kusini. Nchi za SADC ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Tanzania, Angola, Malawi, Zambia, Namibia, Zimbabwe, Botswana, Mozambique, Swaziland, Afrika Kusini, na Lesotho.

Jumuia hii ya SADC inakadiriwa kuwa na jumla ya wakazi milioni 230. SAPP iliundwa mnamo 1995 kwa lengo la kutatua matatizo ya uhaba wa umeme miongoni mwa nchi wanachama wa SADC .

Lakini katika wakati ambapo mtu atauliza vipi nchi kama vile Tanzania, DRC zitaendesha uanachama wake hasa kwa suala ya Miradi ya umeme maana nchi hizi zipo katika SADC na sasa NBI, Tanzania kwa mfano haijajiunga kikamilifu katika Mradi huu wa SAPP.

Mashirika ambayo hayajajiunga kikamilifu katika SAPP ni Shirikala Umeme la Malawi ESCOM, Empresa Nacianal de Electricidade ENE la Angola, na Shirila la Umeme Tanzania TANESCO.

Na mradi huu pia unaendeshwa kwanza na michango ya nchi wanachama lakini pia kwa ufadhili wa Serikali ya Norway kupitia mradi wake wa (NORAD), shirika la Sweden la Sida, Benki ya Dunia, na mashirika mengine kama vile USAID, DFID, na DANIDA.

Nchi hizi hata hivyo zimekuwa hazifikikii kiwango cha uzalishaji umeme kilichotarajiwa na mahitaji ya umeme katika nchi hizi yanazidi kuongezekka kila mwaka.

Kwa mfano ENE la Angola ambalo miundombinu ambayo ilipaswa kuzalisha mw 742, lakini mwaka 2004 lilizalisha mw 374, mwaka 2005 mw 397, na mwaka jana 2006 megawati 432.

Hata lile shirika kubwa la Afrika kusini la ESKOM ambalo linapaswa kuzalisha mw 42,011 mwaka 2004 lilizalisha mw 34,195 mwaka 2005 mw 33,461 na mwaka jana mw 34,807.

Tanzania kwa upande wake ambayo inapaswa kuzalisha mw 897, mwaka 2004 ilizalisha mw 509, 2005 531 na mwaka jana 567.

Umeme unaopaswa kuzalishwa nchini Tanzania kutokana na nguvu za maji ni mw 4,700 mkaa unaokisiwa kupatikana katika hifadhi ardhini ni Tani milioni 15,000 na gesi songosongo ni 1Tcf na Mnazi bay ni 0.5 Tcf.

Kwa upande wa nguvu za nishati inayojulikana kama renewable energy ambayo huzalishwa kutokana na nishati ya jua na upepo inapatikana kwa wingi hapa Tanzania. Mfano nguvu ya jua inapatikana kwa kiwango cha 4.5kWm2/day wakati kiwango cha upepo kinachokutikana maeneo mengi ya Tanzania ni 3-9.2 m/s

Ingawa shirika la Tanesco lililoanzishwa mwaka 1930 yakiwa makampuni mawili na baadae kuwa kampuni moja yenye kumilikiwa na serikali kwa asilimia 100 mwaka 1964 limekuwa likipokea lawama kubwa kutoka kwa wananchi ambao wanaliona kama shirika lililoshindwa kutimza adhma yake ya kuhakikisha wananchi na wafanya biashara nchini wanapatiwa umeme wa kutosha.

Umeme uliopaswa kuzalishwa na shirika hili ni alau mw 897 kama bwawa la Mtera lingezalisha mw 80, Kidatu mw 200 Nyumba ya MUNGU 8, Hale 21, Pangani 68, Kihansi 180, mashine za diezeli 40, songas 200 na IPTL 100.

Hadi mwezi November mwaka 2006 wateja wa umeme nchini Tanzania walikuwa wamefikia 618,000. baadhi wanasema kiwango kilichozalishwa na shirika hilo kwa mwaka 2006 ni mw 583.

Tanesco ina jumla ya wafanyakazi 4,900 na pesa zinazokusanywa na shirika hili ni sh. 25.0 bilioni kwa mwezi.

Ni kwa mtazamo huu baadhi ya wakosoaji wanaonya kuwa kuna nchi katika umoja huu wa NBI ambazo zitanufaika sana na mradi huu wa kuunganisha umeme kutoka nchi moja kwenda nyingine kwani zile zitakazoweza kuzalisha umeme wa ziada zitakuwa zikifanya biashara kwa urahisi.

Kwa mfano Bwana Abdurahman Abu Maali afisa mipango wa National Electric Co-operation ya Sudan Mjini Khartoum aliimbia DW kuwa ingawa nchi yake inahitaji megawati 1000 kwa mwezi lakini alau inazalisha taklibani mw 800.

Lakini pia anapinga wazo kuwa mpango huu utazinufaisha baadhi ya nchi hasa zile zenye nafasi kubwa na majaliwa ya rasilimali nyingi za kuzalisha umeme.

“ hapana sio hivyo Misri pia inategemea kwa asilimia 80 umeme unaozalishwa kutokana na mafuta na unajua nishati hii yapanda na kushuka kila mara dunia nzima, kwa hiyo wakipata umeme nafuu unaozalishwa kutokana na maji kutoka Ethiopia kutoka Sudan hata kutoka kongo, watautumia huo.

na kwa vile Misri imeunganishwa na nchi nyingine kama vile za bara la Ulaya na sisi tutakuwa sehemu ya Dunia nzima”, anasisitiza Bwana Abu Maali.

Lakini pia ikiwa miradi hii itafanikiwa haitakuwa ni faida tu ya umeme, kilimo na kutunza mazingira bali hata kumalizika enzi ya vita baridi vya maji ya Mto Nile vilivyokuwepo baina ya nchi hizi nilizotangulia kuzitaja.

Hii ni kutokana na misri kuzuia nchi nyingine wanachama kuanzisha miradi mikubwa ambayo ingetumia kiaisi kikubwa cha maji ya mto Nile au ziwa Victoria kwa maana kuwa kufanya hivyo kungahatarisha usalama wa Misri.

Kumekuwepo na mazungumzo ya chini kwa chini juu ya utata huu na katika mkutano huu wa Bagamoyo nilimuuliza waziri wa maji wa Tanzania Dk. Shukuru Kawambwa ikiwa mgogoro huo umefikia hatua gani?

“ yah suala hilo tunalizungumza katika ushirika wetu wa nchi kumi. Hiyo inaendana na mikataba ambayo nchi ya Misri imeishawahi kuwekeana na Uingereza katika miaka ya nyuma ili kuhakikisha kwamba wao wanapata maji

Tunachokitambua ni kwamba Misri wanautegemea mto Nile peke yake hawana mito mingine ambayo inaingia kule, kwa hiyo ukizungumzia maji kwa Misri au kwa Sudan unazungumzia maisha ya taifa la Misri na maisha ya taifa la Sudan.

Lakini pia ni kwamba mikataba ile ambayo iliwapa Misri uwezo wa kutumia maji kwa kiasi kikubwa sana ni mikataba ambayo walisaini na wakoloni wetu watu ambao walitutawala Tanzania Kenya na Uganda.

kwa maana nyingine ni kwamba baada ya uhuru haiwezekani tena tukaendelea kuzungumzia mikataba ile kwa sababu ni kama vile kusema nchi hizi bado ni watumwa, wako chini ya Uingereza

kwa hiyo wakati tunaelewa kwamba kwa Misri maji ya mto nile ndio maisha, ukikata maji ya mto nile manake unafuta misri katika ramani au unaifuata Sudani katika ramani ya ulimwengu

lakini pia tunaelewa kwamba mikataba ile ilikuwa ya wakoloni, tukisema tuifate manake ni kwamba Tanzania bado sio huru Kenya sio huru Uganda sio huru” anasema waziri Kawambwa ingawa anaendelea kufafanua kuwa mazungmzo yenye lengo la kumaliza utata huu yanaendelea na yamefikia hatua nzuri.

“Hiyo process tunaendelea nayo, tunaenda vizuri tunaongea vizuri hatujafikia mwisho lakini matumaini makubwa yapo ya namna ya kuelewana namna ya kufanya matumizi ya maji ya mto Nile pamoja pia na kutunza vyanzo vinavyoleta maji katika mto nile na ziwa Victoria” anasisitiza waziri.

Mkataba huo baina ya Misri na Uingereza uliwekwa mwaka 1929 ambapo Uingereza iliahidi kwa niaba ya nchi ilizokuwa ikizitawala kupunguza matumizi ya maji kutoka Ziwa Victoria kwa lengo la kutoiathiri Misri.

Mkataba huo kwa hiyo unazitaka Tanzania Kenya na Uganda kutotumia maji hayo bila idhini ya Misri nchi iliyo umbali wa zaidi ya kilomita 6,000 kutoka eneo la Afrika Mashariki.

Misri hutegemea maji ya mto Nile kwa asilimia 98 kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji. Kwa lugha nyingine maisha ya wakazi wapatao milioni 70 wa nchi hiyo wanategemea maji ya ziwa Victoria na mto Nile.

Mwisho.