1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi zinazoendelea zashikilia madai yao kwa mazungumzzo ya WTO.

Mohamed Dahman12 Juni 2007

Nchi zinazoendelea zimeapa hapo jana kutetea msimamo wao juu ya masuala ya msingi katika mazungumzo ya biashara duniani yaliokwama ikiwa ni wiki moja kabla ya wahusika wanne wakuu wa Shirika la Biashara Duniania WTO kufanya jaribio jengine la kukwamuwa mazungumzo hayo.

https://p.dw.com/p/CHkc
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Biashara Duniani WTO Pascal Lamy akitafakari jambo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Biashara Duniani WTO Pascal Lamy akitafakari jambo.Picha: AP

Waziri wa mambo ya nje wa Brazil Celso Amorim amesema baada ya kukutana na mawaziri wenzake na maafisa kutoka mataifa mengine yanayoendelea mjini Geneva kwamba wanaendelea kushikilia msimamo wao huo wa pamoja.

Amesema wote wanajuwa kwamba wako kwenye awamu ya kuzungumza lakini hawataki kuitolea muhanga misimamo yao ya msingi kwa ajili tu ya kupata matokeo ya haraka.

Mkutano wa Jumatatu katika makao ya Shirika la Biashara Duniani mjini Geneva Uswisi umewahusisha takriban wawakilishi 100 kutoka kundi la mataifa 20 (G20) ya nchi zinazoendelea na zile zinazoinukia kiuchumi katika Shirika la Biashara Duniani WTO kadhalika nchi wanachama wa makundi mengine ya nchi zinazoendelea.

Makundi hayo yamesisitiza katika taarifa kwamba kilimo ni kitovu cha Makubaliano ya Maendeleo ya Doha ambayo yamezinduwa mazungumzo ya biashara duniani katika mji huo mkuu wa Qatar hapo mwaka 2001.

Mkutano wa mawaziri kutoka Brazil,Umoja wa Ulaya, India na Marekani katika mji wa Postdam Ujerumani wiki ijayo unatarajiwa kufanya jaribio jengine la kukwamuwa mazungumzo ya miaka mitano ya Shirika la Biashara Duniani WTO yaliokumbwa na misuko suko.

Mataifa hayo manne yanawakilisha maslahi ya nchi mbali mbali za kimaskini na kitajiri katika Shirika la Biashara Duniani WTO.Makubaliano miongoni mwao juu ya maafikiano yanayohitajika katika kupunguza vikwazo kwenye biashara ya kilimo,bidhaa za viwanda na huduma inaonekana kuwa ni muhimu katika kuzivutia nchi wanachama 150 zilizobaki.

Waziri wa biashara wa India Kamal Nath mshirika mkuu wa Amorin waziri wa mambo ya nje wa Brazil amesisitiza kwamba Duru ya Doha kimsingi imekusudia kutumia biashara kuzisaidia nchi maskini.

Amewaambia waandishi wa habari kwamba maudhui ya duru hiyo ni muhimu zaidi kuliko muda wa kumaliza mazungumzo hayo na kwamba wanaamini kuwa hiyo ni fursa ya kihistoria kusahihisha kasoro za muudo katika biashara ya kilimo.

Mataifa yanyoendelea na mataifa ya kitajiri kwa kiasi kikubwa wanatafuatiana juu ya kiwango cha msaada wa serikali kwa masoko ya kilimo sambamba na kiwango cha ulindaji masoko dhidi ya bidhaa zinazoingizwa kutoka nje hususan katika Umoja wa Ulaya na Marekani.

Mataifa ya kitajiri pia yanataka ridhaa zaidi kutoka nchi zinazoendelea ili kupatiwa nafasi katika masoko yao ya bidhaa za viwandani au kwa makampuni ya kutowa huduma.

Nchi zinazoendelea kwa upande wao zimeitaka Marekani kupunguza msaada wake kwa wakulima wa ndani ya nchi wa dola bilioni 22 kwa mwaka hadi kuwa dola bilioni 12.

Kundi la Mataifa Manane lenye maendeleo makubwa ya viwanda duniani G8 hapo Ijumaa limetowa wito wa kufikiwa kwa maendeleo ya haraka katika Duru ya Doha.

Nchi wanachama 150 wa Shirika la Biashara Duniani WTO zinatumai kufikia makubaliano mwishoni mwa mwaka huu lakini huko nyuma ziliweka tarehe za mwisho kama hizo kukamilisha makubaliano hayo bila ya mafanikio.