1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege ya Malaysia bado ni kitendawili

Admin.WagnerD8 Machi 2016

Wachunguzi wanaotaka kujuwa kile kilichoisibu ndege ya shirika la ndege la Malaysia safari nambari MH370 wamesema sababu ya kutoweka kwa ndege hiyo bado ni kitendawili wakati ikitimia miaka miwili tokea kutoweka kwake.

https://p.dw.com/p/1I94x
Watu wakiandika ujumbe kuwakumbuka wahanga wa ndege ya Malaysia iliotoweka Kuala Lumpur. (08.03.2016)
Watu wakiandika ujumbe kuwakumbuka wahanga wa ndege ya Malaysia iliotoweka Kuala Lumpur. (08.03.2016)Picha: picture-alliance/dpa/F. Ismail

Timu ya kimataifa ya wataalamu wa safari za anga iliyoundwa kuchunguza kisa cha kutoweka kwa ndege hiyo imetowa repoti ya kila mwaka yenye kuelezea hatua zilizopigwa lakini taarifa yao fupi haina maelezo ya kina juu ya kile kilichosababisha kutoweka kwa ndege hiyo.

Mkuu wa timu hiyo ya uchunguzi Kok Soo Choon alisoma taarifa hiyo kwenye televisheni mjini Kuala Lumpur Jumanne (08.03.2016)

Choon amesema "Kwa wakati huu timu ya uchunguzi inaendelea kukamilisha uchanganuzi wake , kile ilichogunduwa, hitimisho, mapendekezo ya usalama kwa maeneo manane husika yanayohusishwa na kutoweka kwa ndege hiyo kwa kuzingatia taarifa zinazostahiki."

Hadi sasa mabaki ya ndege hiyo bado hayakupatikana licha ya kuendelea kutafutwa kusini mwa bahari ya Hindi.

Matumaini bado yangalipo

Hata hivyo Malaysia na Ausralia zimesema bado zinaendelea kuwa na matumaini kwamba juhudi zao za kuitafuta katika eneo la bahari ya Hindi inakoaminika imeangukia zitapelekea kujulikana kwa kitu fulani katika data za kurekodi safari ya ndege hiyo na hatimae kubainisha kile kilichosababisha kutoweka kwake miaka miwili iliopita siku kama ya leo.

Waziri Mkuu wa Malaysia Najib Razak.
Waziri Mkuu wa Malaysia Najib Razak.Picha: picture-alliance/dpa/F. Ismail

Wabunge wa Malaysia Jumanne wamebaki kimya kwa dakika moja kuwakumbuka abiria na wafanyakazi wanaohofiwa kupoteza maisha katika kisa hicho.

Waziri Mkuu wa Malysia Naijib Razak amesema katika taarifa uchunguzi wa hivi sasa wa kuitafuta ndege hiyo unatarajiwa kukamilika baadae mwaka huu na kwamba wanendelea kuwa na matumaini ndege hiyo safari ya MH370 ya Malaysia itapatikana.

Uthibitisho wa kuanguka kwa ndege

Ubawa wa ndege hiyo uliopatikana mwezi wa Julai mwaka jana katika visiwa vya Reunion ni ushahidi pekee unaothibitisha kwamba ndege hiyo imeanguka juu ya kwamba Malaysia inachunguza vipande vyengine viwili vipya mabaki ya ndege yaliokutikana visiwa vya Reunion na Msumbiji.

Zamani Zakaria amempoteza mke na mtoto wake wa kiume waliokuwemo katika ndege iliyotoweka Kuala Lumpur. (08.03.2016)
Zamani Zakaria amempoteza mke na mtoto wake wa kiume waliokuwemo katika ndege iliyotoweka Kuala Lumpur. (08.03.2016)Picha: picture-alliance/dpa/F. Ismail

Familia zilizopoteza ndugu na jamaa zao Jumanne zimeandamana mjini Beijing China kushinikiza kutatuliwa kwa kitendawili cha kuanguka kwa ndege hiyo.

Dai Shukin ambaye dada yake na familia yake walikuwemo katika ndege hiyo iliyotoweka amesema "Hatujuwi iwapo wako hai au wamekufa.Hatujuwi wako katika hali gani mbaya au nzuri.Tuna wasi wasi mkubwa sana.Tuna msongo wa kisaikolojia aina fulani ya chuki na dhiki."

Ndege hiyo ya Malaysia ilitoweka Machi 8 mwaka 2014 ilipokuwa safarini kutoka Kuala Lumpur kuelekea Beijing ikiwa na abiria 239 na wafanyakazi wengi wao wakiwa ni raia wa China na Malaysia.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman