1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege yadunguliwa rubani atekwa Syria

28 Novemba 2012

Waasi nchini Syria wamemteka nyara rubani wa ndege ya serikali baada ya kuidungua ndege hiyo ya kijeshi katika eneo la Daret Ezza Kaskazini mwa mkoa wa Allepo. Mabomu yaua kiasi ya watu 34 Damascus.

https://p.dw.com/p/16sAH
-
-Picha: Reuters

Shahidi aliyezungumza na shirika la habari la Afp kwenye mji wa Tourmanin ulioko kilomita moja kutoka Daret Ezza anasema marubani wawili walitumia miavuli kuruka kutoka kwenye ndege hiyo baada ya kudunguliwa.Mmoja kati ya marubani hao aliwekwa kizuizini..

Halikadhalika mashambulio mawili ya mabomu ya kutegwa ndani ya gari yameutikisa mji wa Jaramana nyumbani kwa kabila la waliowachache nchini Syria la Druze pamoja na wakristo waliokimbia vita kutoka maeneo mengine ya nchi.Maduka pamoja na majengo mengine yameharibiwa vibaya kutokana na mashambulio hayo ya mji huo ulioko Damascus.Shambulio hilo ndiyo baya kabisa kuwahi kushuhudiwa katika mji mkuu huo ndani ya kipindi cha miezi mingi.Hata hivyo kutokana na hatua ya serikali ya kuzuia vyombo vingi vya habari vya kujitegemea kuingia nchini Syria haikuwa rahisi kuweza kuthibitisha juu ya ripoti za mashambulio hayo ingawa serikali inasema watu 34 wameuwawa.

Shambulio la Bomu Damascus
Shambulio la Bomu DamascusPicha: picture alliance/dpa

Mashambulio hayo yanafuatia wiki mbili za kuongezeka kwa nguvu za waasi ambao wamevamia na kuziteka kambi kadhaa za kijeshi kote nchini na kuonesha jinsi gani utawala wa Assad ulivyopoteza udhibiti wa eneo la Kaskazini na Mashariki licha ya kutumia ndege zake za kijeshi kushambulia ngome za waasi. Katika tukio jingine la kuonesha kuimarika nguvu za waasi kufuatia kujipatia silaha kufuatia uvamizi walioufanya dhidi ya taasisi za kijeshi pamoja na kupokea nyingine kutoka nchi za nje,wapiganaji wameidungua ndege ya kivita katika mkoa wa Aleppo wakitumia Kombora la kudungua ndege.

Taarifa hizo zimesambazwa na kundi la kusimamia masuala ya haki za binadamu la Syria huku ikionyesha video kupitia mtandao wa You Tube inayoonyesha picha za mtu akivuja damu kwa wingi katika sehemu yake ya kichwani na kuonekana akiwa katika hali mbaya.Sauti iliyosikika kwenye video hiyo inasema kwamba mtu huyo ni rubani wa ndege iliyodunguliwa aliyekuwa akishambulia kutoka angani majumba ya raia.

Video nyingine ilionyesha ndege ya kijeshi iliyoteketea.Umwagikaji huo wa damu umekuja wakati ambapo muungano wa upinzani ukiwa umefanya mazungumzo kamili ya kwanza mjini Cairo hii leo kujadili juu ya kuunda serikali ya mpito ambayo ni muhimu katika kupata uungaji mkono wa nchi za Kiarabu na zile za Magharibi katika harakati za kumuondoa madarakani Assad na Utawala wake

Aleppo yaendelea kushambuliwa
Aleppo yaendelea kushambuliwaPicha: Reuters

.Mmoja kati ya makamu wa rais wawili katika muungano huo Suhair al-Attas amenukuliwa kusema kwamba lengo ni kuchaguliwa waziri mkuu atakayeiongoza serikali hiyo ya mpito au alau orodha ya watakaogombea nafasi hiyo.Mkutano huo utamalizika kesho na pia utahusika katika kuichagua kamati itakayosimamia masuala ya misaada na mawasiliano. Aidha mvutano unaongezeka kati ya wapinzani walioko uhamishoni na waasi walioko katika mapambano ndani ya Syria ambako idadi ya waliouliwa imefikia watu 40,000 wakiwemo wanajeshi,raia na waasi.

Mwandishi :Saumu Mwasimba/Reuters/AFP

Mhariri:Mohammed AbdulRahman