1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege za Israel zashambulia Syria

4 Mei 2013

Israel imefanya shambulio la anga dhidi ya shehena ya makombora ya Syria yaliokuwa yakisafirishwa kupelekwa kwa kundi la wapiganaji wa Hezobollah lilioko katika nchi jirani ya Lebanon.

https://p.dw.com/p/18SLF
Jeti ya Israel
Jeti ya IsraelPicha: picture-alliance/dpa

Israel ilikuwa imesema kwa muda mrefu kwamba iko tayari kutumia nguvu kuzuwiya silaha za kisasa na zile za sumu za utawala wa Rais Bashar al-Assad kuwafikia washirika wao wa kundi la itikadi kali za Kiislamu la Hezbollah au waasi wengine wa itikadi kali za Kiislamu wanoshiriki katika uasi wa miaka miwili dhidi ya serikali ya nchi hiyo.

Hezbollah kwa kushirikiana na Iran adui mkubwa wa Israel waliendesha vita vilioshindwa kutoa mshindi dhidi ya taifa hilo la Kiyahudi hapo mwaka 2006 na linaendelea kuwa tishio kubwa machoni mwa Israel.

Waasi wa itikadi kali za Kiislamu inahofiwa kwamba wanaweza kuzielekeza silaha zao dhidi ya Israel baada ya miongo minne ya kuwepo utulivu wa wastani katika eneo la mpaka la Milima ya Golan.

Shabaha sio silaha za sumu

Duru za usalama katika kanda hiyo hapo awali zimesema kwamba shabaha ya shambulio hilo la Ijumaa ilikuwa sio kituo cha silaha za sumu cha Syria.Afisa wa serikali ya Israel aliyekataa kutajwa jina amekiri kutokea kwa shambulio hilo.

Mwanamke alieathirika na silaha za sumu katika mji wa Allepo nchini Syria.
Mwanamke alieathirika na silaha za sumu katika mji wa Allepo nchini Syria.Picha: Reuters

Kwa mujibu wa duru hizo za usalama,shambulio hilo limekuja baada ya baraza la usalama la mawaziri la Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuliidhinisha katika mkutano wa faragha Alhamisi usiku.Afisa wa serikali ya Marekani ambaye pia alikataa kutajwa jina ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba shambulio hilo lililenga jengo moja.

Maafisa wa serikali ya Lebanon waliripoti kuwepo kwa harakati nzito zisizo za kawaida za kikosi cha anga cha Israel juu ya anga yao hapo Alhamisi na Ijumaa.Duru za usalama za Lebanon zimesema dhana yao kwanza ilikuwa ni kwamba ndege hizo za Israel zilikuwa zikichunguza usafirishaji wa silaha kati ya Syria na Lebanon na hususan silaha hizo kuepelekewa kundi la Hezbollah.

Balozi wa Syria kwa Umoja wa Mataifa Bashar Ja'aafari ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba hana habari juu ya shambulio hilo.

Msafara wa silaha

Lakini Qassim Saadedine kamanda na msemaji wa Jeshi Huru la Syria amesema habari walizonazo zinadokeza kwamba kumekuwepo na shambulio la anga la Israel kwa msafara wa magari uliokuwa ukisafirisha makombora kupelekea kundi la Hezbollah lakini bado hawakujuwa juu ya mahala pa shambulio hilo.

Wapiganaji wa Jeshi Huru la Syria.
Wapiganaji wa Jeshi Huru la Syria.Picha: Reuters

Vikosi vya waasi vinatofautiana juu ya aina za aina silaha ziliokuwemo kwenye msafara huo ambapo habari nyengine za kijasusi zinasema yalikuwa ni makombora ya kudungulia ndege.

Kwa mujibu wa muasi mmoja aliekataa kutajwa jina kulikuwepo na mashambulizi matatu ya ndege za kivita za Israel F-16 ambazo zimeangamiza msafara wenye kubeba makombora hayo ya kudungulia ndege yaliokuwa yakipelekwa kwa kundi la Hezbollah katika barabara ya kijeshi ilioko kati ya Damascus na Beirut.

Shambulio jengine linatajwa kufanyika karibu na eneo moja la Kikosi cha Nne cha Vifaru cha Syria huko al-Saboura lakini haikuweza kubainishwa kulikuwa na kitu gani katika eneo hilo.

Hapo mwezi wa Januari mwaka huu Israel iliushambulia kwa mabomu masafara wa magari nchini Syria ambapo iliaminika kuwa ulikuwa na silaha zilizokuwa zikipelekwa kwa kundi la Hezbollah ingawa Israel yenyewe haikukiri rasmi kufanya shambulio hilo.

Wakimbia kuhofia kuuwawa

Wakati hayo yanajiri mamia ya Waislamu wa madhehebu ya Sunni wameukimbia mji wa mwambao wa Banias Jumamosi (04.05.2013) kwa kuhofia kuzuka kwa ghasia zaidi za kimadhehebu baada ya wapiganaji walio tiifu kwa Rais Bashar al-Assad kuwaua watu chungu nzima wakati wa usiku.

Wakimbizi wa Syria wakiwa katika makambi.
Wakimbizi wa Syria wakiwa katika makambi.Picha: picture-alliance/dpa

Wanaharakati wamesema mauaji katika kitongoji cha Ras al-Nabaa cha mji wa Banias yalifanyika siku mbili baada ya vikosi vya serikali kuuwa takriban Wasunni 50 katika kijiji cha jirani cha Baida.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri: Caro Robi