1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni shambulizi la la 39 dhidi ya kituo cha afya

28 Oktoba 2015

Hakukuwa na mtu ndani ya jengo wakati lilipotokea shambulio la pili lililolilenga jengo moja la karibu na mahala hapo. Dakika 10 baadae wakalazimika kuwahamisha wahudumu na wagonjwa wapatao 10.

https://p.dw.com/p/1GvJh
Jemen Houthi Rebellen Trümmer Ruine Luftangriff Saudi Arabien
Picha: picture-alliance/dpa/Y. Arhab

Mashambulizi ya ndege za kivita za muungano wa kijeshi unaongozwa na Saudi Arabia yakiwalenga waasi nchini Yemen, yameiharibu hospitali inayoongozwa na Shirika la Madakatari wasio na Mipaka-MSF katika wilaya ya kaskazini ya Saada. Taarifa imesema hakukuwa na vifo lakini mtu mmoja alijeruhiwa.

Kiongozi wa ofisi ya Shirika hilo nchini Yemen Hassan Boucenine aliliambia Shirika la habari la Associated Press-AP kutokea mji wa bandari kusini mwa nchi hiyo wa Aden kwamba, shambulizi la kwanza lilifanyika Jumatatu asubuhi na kuliharibu jengo lenye ofisi za utawala za MSF. Hakukuwa na mtu ndani ya jengo wakati lilipotokea shambulio la pili lililolilenga jengo moja la karibu na mahala hapo. Dakika 10 baadae wakalazimika kuwahamisha wahudumu na wagonjwa wapatao 10.

Afisa huyo alisema mashambulizi ya mabomu limekuwa jambo la kawaida na kwamba shambulizi hilo dhidi ya jengo la Shirika la Madaktari wasio na Mipaka linaashiria kuwa wahusika hawajali kabisa usalama wa raia, akiongeza kwamba kushambuliwa raia ni hospitali ni ukiukaji wa sheria ya kimataifa inayohusika na binaadamu.

Shirika hilo linatoa huduma za matibabu katika wilaya nane, katika wakati ambapo mashirika mengi ya misaada ya kigeni na wafanyakazi wa Umoja wa mataifa wamehamishwa kutoka Yemen . Katika taarifa yake Shirika la MSF limesema hospitali ilioharibiwa ilikuwa ikiwapatia matibabu wagonjwa 3,400 tangu lilipoanza shughuli zake mwezi Mei.

Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ukiungwa mkono na Marekani, umekuwa ukifanya mashambulizi dhidi ya waasi wa Kishia wanaojulikana pia kwa jina la Huthi pamoja na washirika wao tangu Mach, wakati wilaya ya Saada ambayo ni ngome kuu ya waasi hao iikihujumiwa vikali kwa mabomu.

Umoja wa Mataifa unasema eneo lililoshambuliwa hivi karibuni ni kituo cha 39 cha matibabu kuharibiwa tokea vita vilipopamba moto miezi saba iliopita na kuongeza kumekuweko na uhaba mkubwa wa mafuta, madawa, umeme na maji hali inayotoa kitisho cha kwamba huenda vituo zaidi vikafungwa. Shirika la Kimataifa la Haki za Binaadamu-Amnesty International, limeyaita mashambulizi hayo yanayoongozwa na Saudi Arabia kuwa uhalifu wa kivita na kutoa wito pafanyike uchunguzi huru.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman ,ap, dpa
Mhariri:Yusuf Saumu