1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege za Marekani zaipiga al-Shabab

Admin.WagnerD30 Desemba 2014

Jeshi la Marekani limefanya shambulizi kumlenga kiongozi wa al-Shabab ambaye hakutajwa jina. Shambulizi hili la Jumatatu limekuja siku chache baada ya kujisalimisha kwa aliyekuwa kinara wa upelelezi wa kundi hilo.

https://p.dw.com/p/1EDDs
Mashambulizi ya anga ya Marekani yalimlenga kiongozi wa al-Shabab ambaye hakutajwa
Mashambulizi ya anga ya Marekani yalimlenga kiongozi wa al-Shabab ambaye hakutajwaPicha: AP

Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la Marekani Admiral John Kirby, kiongozi aliyelengwa katika shambulio hilo sio kamanda mkuu mpya wa al Shabab Ahmad Umar, ambaye amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Ahmed Abdi Godane aliyeuawa katika shambulizi jingine la Marekani la tarehe moja mwezi September.

Kiongozi mkuu wa sasa wa al Shabab anajulikana kwa majina mengi ya bandia, lakini maafisa wa kijasusi nchini Somalia wanasema wanamfahamu kama Sheikh Mahad Abdikarim ambaye aliwahi kuwa gavana wa al Shabab katika mkoa wa Bakool.

Siku chache kabla ya shambulizi hilo la jana, mtu ambaye anaaminika kuwahi kuwa mkuu wa ujasusi wa kundi la al Shabab Zakariya Ismail Ahmed Hersi alijisalimisha kwa jeshi la serikali ya mjini Mogadishu na vikosi vya Umoja wa Afrika vinavyoisaidia serikali hiyo dhaifu ambayo lakini inatambuliwa kimataifa.

Marekani ilikuwa imeahidi zawadi ya dola milioni tatu kwa mtu yeyote ambaye angesaidia kukamatwa kwa Zakaria Hersi.

Licha ya kuandamwa kimataifa, al-Shabab imeendelea kujizatiti
Licha ya kuandamwa kimataifa, al-Shabab imeendelea kujizatitiPicha: picture alliance/AP Photo/Sheikh Nor

Hakuna hasara kwa raia

Aidha, katika tangazo fupi lililochapishwa na wizara ya ulinzi ya Marekani kuhusiana na shambulizi la jana, wizara hiyo imesema eneo lililoshambuliwa linajulikana kama Saakow, na kuongeza kuwa ilikuwa na imani kuwa hakuna raia wala mpita njia aliyeuawa au kujeruhiwa katika shambulizi hilo. Tangazo hilo fupi liliendelea kueleza kuwa kwa sasa, Marekani inaendelea kufanya tathmini juu ya matokeo ya shambulio lake dhidi ya al Shabab.

Ikiwa shambulizi hilo litakuwa limefanikiwa kumuuwa kiongozi mwingine muhimu wa al Shabab itakuwa pigo kubwa kwa kundi hilo lenye mafungamano ma mtandao wa kigaidi wa al Qaida, ambalo linataka kuanzisha utawala wa sheria za kiislamu nchini Somalia.

Al-Shabab yajizatiti

Licha ya kuandamwa na makundi ya kimataifa, al Shabab imeweza kustahimili vishindo na kujizatiti mnamo siku za hivi karibuni. Alhamis wiki iliyopita ilifanya shambulizi kali kwenye ngome za vikosi vya Umoja wa Afrika yenye ulinzi mkali, na kuwauwa wanajeshi watatu pamoja na wafanyakazi wengine wanne wa kiraia.

al-Shabab inalaumiwa kwa mashambulizi mengi yenye umwagaji damu nchini Somalia
al-Shabab inalaumiwa kwa mashambulizi mengi yenye umwagaji damu nchini SomaliaPicha: Reuters/F. Omar

Mashambulizi mengine ya kundi hilo mnamo miezi ya hivi karibuni yamekuwa yakilenga vituo muhimu vya serikali na maeneo yenye ulinzi mkali, katika kile kinachooneka kama kukanusha madai ya serikali ya Somalia pamoja na Umoja wa Afrika kwamba kundi hilo liko karibu kutokomezwa.

Tangu kupelekwa nchini Somalia mwaka 2007, kikosi cha Umoja wa Afrika chenye wanajeshi 22,000 kimefanikiwa kuifurusha al Shabab kutoka mjini Mogadishu, na kuisukuma nyuma kutoka ngome zake nyingine muhimu, lakini bado kundi hilo linayadhibiti maeneo makubwa katika mikoa ya kusini na katikati ya Somalia.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ap/afp

Mhariri: Iddi Ssessanga