1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndoto ya kuwa na sarafu moja Afrika Mashariki

14 Aprili 2016

Jumuiya ya Afrika Mashariki inaadhimisha miaka 10 tangu kuanzisha umoja wa forodha uliochangia katika kustawisha uchumi wa nchi wanachama. Biashara imeongezeka lakini bado kuna changamoto.

https://p.dw.com/p/1IVEC
Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Picha: picture-alliance/dpa/Xinhua

Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki inaendelea kustawi. Mnamo mwezi uliopita jumuiya hiyo iliongeza mwanachama wa sita, yaani Sudan Kusini. Jumuiya hiyo imeziwezesha nchi za Afrika mashariki kukaribiana zaidi. Mshauri wa masuala ya kiuchumi kwenye baraza la biashara na viwanda nchini Tanzania, Dirk Smelty, amearifu kwamba kati ya mwaka wa 2005 na 2014 biashara iliongezeka kwa asilimia 300 baina ya nchi wanachama, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi na Tanzania.

Na mnamo mwaka wa 2005 nchi hizo zilianzisha Umoja wa forodha, na kuanzia mwaka wa 2010 nchi hizo zilikubaliana juu ya kupunguza vizingiti baina yao. Watu wao wanaweza kusafiri na kufanya kazi katika nchi yoyote mwanachama kwa urahisi. Wajasirimali wanaweza kuchagua kufanya biashara wanakopenda.

Kwa mujibu wa ripoti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, tangu kuanzishwa kwa Umoja wa forodha Kenya na Uganda zimeweza kuongeza madahuli mara nne na Tanzania mara nne. Hata hivyo biashara baina ya Rwanda na Burundi imeendelea kuwa ya kiwango cha chini. Hata hivyo mtaalamu wa masuala ya kiuchumi James Shikwati ameeleza kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki inazidi kupiga hatua mbele. "Katika sekta ya uchumi jumuiya inaendelea kujengeka. Hata katika mipango yao ya biashara wafanyabiashara wanapiga hesabu juu ya watu Milioni 148 wa eneo hili. Mabenki yanafunguliwa katika eneo hilo na maduka makubwa kadhalika"

Marais wa Rwanda na Tanzania: Paul Kagame na John Magufuli
Marais wa Rwanda na Tanzania: Paul Kagame na John MagufuliPicha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Miundombinu zaidi yahitajika

Tanzania iliyokuwa inasuasua hapo awali sasa haifungi breki zote. Lakini mguu wake bado uko kwenye breki. Licha ya ustawi thabiti wa uchumi Tanzania bado haijaingia kichwa mbele katika utangamano wa kiuchumi!

Nchi hiyo bado inapima urefu wa maji kwa ujiti. Lakini tangu Rais John Magufuli aingie madarakani ishara mpya zimeonekana juu ya kuimarisha ushirikiano. Juu ya kuimarisha ushirikiano huo mshauri wa masuala ya kiuchumi Smelty amesema bado pana hatua muhimu zinazopaswa kuchukuliwa.

Miundombinu katika maeneo mengi yahitaji kuboreshwa
Miundombinu katika maeneo mengi yahitaji kuboreshwaPicha: Getty Images/AFP/J. Vaughan

Amesema jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki inahitaji kujenga miundombinu. Ameeleza kuwa barabara pia lazima zipanuzwe na ziongezwe.

Wakati huo huo Jumuiya ya Afrika mashariki inayo malengo makubwa zaidi mbali na kujenga miundombinu. Tangu mwaka wa 2010 pana mipango ya kuanzisha sarafu ya pamoja. Lakini jee lengo hilo litafikiwa katika muktadha wa migogoro katika nchi wanachama? Sudan Kusini, mwanachama mpya, bado imo katika machafuko na Burundi bado inakabiliwa na mgogoro wa kisiasa.

Mwandishi: Theresa Krinninger

Mfasiri: Abdu Mtullya

Mhariri: Josephat Charo