1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nepal kuwa jamhuri ?

Saumu Mwasimba24 Desemba 2007

Serikali ya mpito yamuonya mfalme Gynadra ikiwa atazuia uchaguzi basi watauondoa ufalme.

https://p.dw.com/p/CfpS
Bunge la NepalPicha: AP

Vyama vikuu vya kisiasa nchini Nepal vimeridhia kuundoa utawala wa kifalme kama sehemu mojawapo ya makubaliano ya kuwarudisha waasi wa zamani wa kikomunisti katika serikali.Ingawa hakuna ratiba iliyowekwa kwa waasi hao kujiunga na serikali makubaliano hayo yaliyotiwa saini jumapili yanatoa nafasi ya kupatikana jamhuri kamili ya Nepal ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja baada ya tangu mfalme Gynadra alipolazimishwa kuondoa utawala wake wa kidikteta kufuatia wiki kadhaa za ghasia katika mji mkuu Kathmandu.

Chini ya makubaliano hayo utawala wa Kifalme utaondolewa na Nepal kutangazwa jamhuri kamili pindi tu uchaguzi mkuu utakapofanyika na kuundwa kwa serikali mwaka ujao.

Akizungumzia kuhusu hatua hiyo mwanachama wa chama cha kikomunisti,Bharat Mohan Adhikari alisema…

''Endapo mfalme akijaribu kuzuia uchaguzi usifanyike basi uwingi wa thuluthi mbili katika serikali hii ya mpito unaweza kuuondoa ufalme na kuitangaza Nepal kuwa Jamhuri.''

Itakumbukwa kwamba waasi wa kimao walijiondoa serikalini mwezi Septemba wakidai utawala wa kifalme uondolewe mara moja.Maafisa wanasema wanataka uchaguzi ufanyike katika awamu ya mwanzo wa mwaka 2008.

Uchaguzi wa bunge ambalo litaweka sawa hatma ya kisiasa ya taifa hilo linalolemewa na umaskini umewahi kuhairishwa mara mbili kufuatia mivutano juu ya mapendekezo ya waliokuwa waasi wakimao ambao walitaka mfumo wa upigaji kura ubadilishwe na ufalme uondolewe mara moja.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa jana badala ya bunge la viti 497 sasa kutakuwa na viti 601.

Kiasi cha wabunge 335 watachaguliwa kupitia mfumo wa uwakilishi kulingana na uwingi wa kura na wengine 240 watachaguliwa kupitia mfumo wa chama kilicho na sauti.Aidha vyama vitateua jumla ya wabunge 26 lakini hapa wachunguzi wa masuala ya kisiasa nchini Nepal wanasema kuna hatari ya waasi wa kimao huenda wakatoa mapendekezo mapya wakati uchaguzi ukikaribia kwasababu hali hiyo imeshawahi kutokea.

Itakumbukwa pia makubaliano ya amani kati ya waasi wa zamani wa kimao na vyama vya kisiasa yalimaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Nepal mwishoni mwa mwaka jana lakini hali imebakia kuwa tete katika eneo la Terai.Kiasi cha watu 200 waliuwawa mapema mwaka huu katika mapigano ya eneo hilo.Hivyo baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaonya hali inaweza kuwa ngumu kuelekea uchaguzi hadi pale mzozo katika eneo hilo ambalo lina ardhi yenye rotuba utakapotatuliwa.